Ofisi ya Msajili wa Hazina inawajengea uwezo watumishi wake katika masuala yanayohusiana na Ubinafsishaji katika mafunzo ya wiki mbili yanayoendelea katika Chuo cha  Uhasibu Arusha, Jijini Arusha. Katika mafunzo hayo watumishi wa Ofisi hiyo watapata elimu, maarifa, ujuzi na uzoefu wa kiutendaji utakaosaidia kuielewa dhana nzima na taratibu za Ubinafsishaji.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto alisema mafunzo hayo yatasaidia kutambua changamoto za ubinafsishaji na namna ya kukabiliana nazo pamoja kupata uelewa mzuri wa kusimamia Taasisi zilizobinafsishwa. Na kwamba mafunzo hayo yanatolewa kama sehemu ya kuimarisha uwezo wa Ofisi katika kutekeleza majukumu ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina ilirithi kutoka  PSRC na CHC ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa ufilisi uliokuwa unaendelea, urekebishaji, ubinafsishaji  wa mashirika ya umma, na ufatiliaji na tathmini ya mali na mashirika yaliyobinafsishwa.

 

“Nafarijika kuona kuwa mafunzo haya yanatokea kwa wakati muwafaka ambapo ofisi yetu inaendelea na zoezi la ubinafishaji wa mashirika 20 ambayo yalirejeshwa serikalini baada ya wamiliki wake wa awali kushindwa kutekeleza mashariti ya mikataba ya mauzo ya mashirika hayo. Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatasaidia kuharakisha na kuboresha zoezi hili linaloendelea” alisema Mgonya.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Msajili wa Hazina katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji, Ufuatiliaji, Tathmini na Utafiti, Mohammed Nyasama alisema malengo ya mafunzo ni kujenga uelewa kuhusu sheria, sera, taratibu na mbinu na mikakati yote inayotumika katika zoezi zima la ubinafsishaji wa mashirika na mali za umma lakini washiriki watapata muda mzuri wa kubadilishana uzoefu kuhusiana na masuala ya ubinafsishaji.  Aidha  Nyasama alisisitiza kuwa mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi katika kufanya uchambuzi unaohusiana na zoezi zima la ubinafsishaji.

Aidha, Msajili wa Hazina amewapongeza wakufunzi pamoja na uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kwa kuandaa mafunzo mazuri na kutumia wakufunzi wabobezi na wenye uelewa na uzoefu mkubwa katika masuala ya Ubinafsishaji