Na Mwandishi Wetu

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano wa kikao kazi baina ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, watendaji na wenyeviti wa taasisi na mashirika ya umma, kinachotarajiwa kufanyika Agosti 19 hadi 21, mwaka huu jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu mkutano huo, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema kikaokazi hicho kitakuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo mada tano muhimu za kuboresha zaidi utendaji wa taasisi hizo.

“Huu utakuwa ni mkutano mkubwa utakaokutanisha watendaji na wenyeviti kwa pamoja kujadili masuala nyeti. Rais Samia ataufungua mkutano huu na anatatoa mwelekeo wa yale anayoyataka,” alisema.

Alisema katika kikao hicho kitajikita katika viongozi hao kukumbusha mambo ambayo wenyeviti na watendaji wanatakiwa kuzingatia katika utendaji wao.

“Kwa sababu tusipokumbushana katika hili ni rahisi kuona mwenyekiti wa bodi anafanyakazi za menejimenti na menejimenti inakuwa kipofu haitambui majukumu ya bodi na kujenga mgogoro usikuwa wa lazima ndio maana tunasema ni lazima kukumbushana,” alieleza Mchechu.

Alisema pia kikaokazi hicho kitapitia maboresho ya usimamizi wa taasisi na kutoa vigezo vya utendaji kazi ambapo taasisi hizo zitapatiwa vigezo vipya vya kufanyia kazi kulingana na sekta husika ya taasisi.

“Sasa kwanini tumetengeneza vigezo vipya, zamani kulikuwa na vigezo ambavyo havijazingatia sekta. Unapomsimamia Tanesco au Muhimbili hawa kazi ni tofauti na hadi vigezo vyao. Hivyo ni lazima vigezo viendane na sekta husika na asili ya taasisi inavyofanya kazi yake,” alieleza.

Aidha, alisema kikaokazi hicho kitapitia na kujadili maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka. “Katika kikao hiki kutakuwa na watu takribani 600 wapo wakurugenzi na wenyeviti. Kwenye zile bodi wapo watu wengi wenye ujuzi na taaluma za uhakika hivyo ni sehemu nzuri ya kulifanyia kazi hili,”

Mchechu alisema kikao hicho pia kitajadili changamoto mbalimbali za taasisi ikiwemo viongozi hao wa taasisi kupatiwa mafunzo ya uongozi ili kuboresha utendaji wa taasisi hizo.

“Hapa tumelenga kukumbushana wajibu wetu, sheria za CAG mambo yanayohitajika na mambo ya maadili na mengineyo,” alisema.

Pamoja na hayo, Msajili huyo alisema kwa kuwa kikaokazi hicho ni cha kwanza pia kutakuwa na utambuzi wa baadhi ya taasisi zilizofanya vizuri na kutakuwa na makundi manne.

Alisema kupitia taasisi za kibiashara ambazo serikali ina hisa nyingi taasisi tano zitatambuliwa kwa kutoa gawio kubwa serikalini na kati ya hizo tanu taasisi tatu zilizofanya vizuri zaidi zitapatiwa tuzo.

Kwa taasisi ambazo serikali ina hisa kuanzia asilimia 50 kushuka chini nazo tano zitatambuliwa kwa kutoa gawio kubwa serikalini na tatu zilizofanya vizuri zitapewa tuzo na taasisi zisizo za biashara zinazochangia asilimia 15 ya gawio nazo tano zitatambuliwa na tatu zilizofanya vizuri zitapewa tuzo.

Mchechu alisema kundi lingine ni kwa taasisi zilizozalisha faida nyingi na kundi la taasisi zilizokuwa zinafanya vibaya halafu zikaanza kufanya vizuri ambazo nazo tano zitatambuliwa na tatu zilizofanya vizuri zitapewa tuzo.

“Mwaka huu kwa kwa tunaanza tutatoa tuzo kwa zile zilizofanya vizuri. Mwakani zilizofanya vibaya nazo zitatambuliwa,” alisema.

Mwenyekiti wa Watendaji wa taasisi na mashirika ya Umma sabasaba Moshingi alisema kikaokazi hicho ni muhimu kwa watendaji hao kwa kuwa wataoata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na hivyo kuboresha zaidi taasisi zao.

Mwisho