Na Mwandishi Maalumu

KATIBU Mkuu Kiongozi, Mhe.Balozi Dkt.Moses Kusiluka amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ina matumaini makubwa na mashirika zikiwemo taasisi mbalimbali za umma katika kutoa huduma bora kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hayo ameyabainisha Agosti 21, 2023 jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Agosti 19, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kikao hicho alisema, Serikali imewekeza fedha nyingi katika mashirika ya umma huku ikiwa haioni tija, hivyo Serikali inatarajia kufanya mabadiliko makubwa.

“Ndugu zangu ma-CEO (Maafisa Watendaji Wakuu), Wenyeviti wa Bodi hatutanii, tumeshatoa fedha nyingi sana, zinaingia kwenye drainage, hatuoni tija yake.

“Sasa ni kuwekeana vigezo, ni kuwekeana vipimo vya utekelezaji au utendaji, lakini kuwekea targets za kufanya faida, ukishindwa huna sababu ya maana, kufa na shirika lako,”alisisitiza Rais Dkt.Samia.

Mbali na hayo, Dkt.Kusiluka akifunga kikao hicho ambacho washiriki walijadiliana mambo mbalimbali kwa ustawi bora wa mashirika na taasisi hizo za umma alibainisha kuwa;

“Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mbalimbali, niungane na wote kumshukuru Mheshimwa Rais kwa maono yake na utashi wake kwamba taasisi za umma na mashirika zinafanyiwa maboresho makubwa ili kuongeza tija.

“Niwaombe mkayasimamie maelekezo ya Mheshimiwa Rais ipasavyo. Kila mtu katika sehemu yake na nafasi yake kazi ya ofisi yangu ni kuhakikisha maelezo ya Mheshimiwa Rais yanatekelezeka kwa ukamilifu nimuahidi Mheshimiwa Rais nitafuatilia na kusimamia kwa karibu.”

Mheshimiwa Balozi Dkt.Kusiluka alifafanua kuwa, mashirika na taasisi za umma ni kiungo muhimu baina ya Serikali na wananchi, hivyo kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali unafanyika kupitia mashirika na taasisi za umma.

“Sote tunatambua kwamba,wananchi wanahitaji huduma bora, kwa sasa bado taasisi nyingi zinatoa huduma duni. Na ni wajibu wa taasisi zote na mashirika ya umma kutoa huduma bora kama vile umeme, afya, maji, elimu na pia ziwe na ubora na ufanisi mkubwa kwa ukamilifu na kwa wakati.

“Na pale inapotokea shida wananchi wanapaswa wafahamishwe shida hiyo na ishughulikiwe kwa haraka, tambueni huu ni wajibu wenu.”

 

Wakati huo huo, Mheshimiwa Balozi Dkt.Kusiluka amebainisha kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu la kusimamia mashirika na taasisi za umma na Serikali kwa sasa hivi inafanyia maboresho taasisi hizo.

“Yapo mageuzi mengi sasa hivi Serikali inayasimamia kwenye Ofisi hii.Lengo ni ofisi hii kusimamia vizuri shughuli za taasisi na mashirika ya umma.

“Na Serikali kwa sasa ipo katika mchakato wa kutunga sheria mpya itakayompatia TR (Msajili wa Hazina) uwezo mkubwa wa kusimamia uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma na taasisi za Serikali.

“Sote tuhakikishe tunashiriki kikamilifu katika mchakato wa utungaji wa sheria hii ili tuwe na sheria bora itakayotuletea tija.

“Natoa wito muipatie ushirikiano Ofisi ya Msajili wa Hazina hatutarajii mkaanza kuikosoa kama unakosoa unakosoa kwa sababu ya kujenga na kwa sababu inaanza inaweza kuwa na dosari moja au mbili.

“Lakini Serikali inakusudia kuwa na ofisi yenye nguvu na tija na wataalamu wa kutosha, pia imarisheni ushirikiano na wizara mama zenu yaani wizara za kisekta.

“Pia, viongozi wa wizara wasiwashinikize kuwalipia huduma ambazo hawastahili, zingatieni sheria na miongozo na kanuni za utendaji kazi serikalini.

“Na huo ndio msingi wa Mheshimiwa Rais pia Rais alielekeza bodi zitumie mamlaka yake kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi husika katika kuziendesha taasisi hizo.

“Hata hivyo ningependa kuwakumbusha kuepuka matumizi mabaya ya madaraka mliyopewa ikiwemo upendeleo wa ajira za watumishi na maamuzi juu ya stahili za viongozi na watumishi. Tuwe makini huko nyuma hatukufanya vizuri juu ya hili.

“Mtakumbuka pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais alielekeza mashirika na taasisi za umma zipitiwe upya kwa lengo la kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuongezea mitaji baadhi ya taasisi na mashirika ya umma.

“Pia kuangalia baadhi ya mashirika na taasisi za umma zingine kuzifuta.Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji inaelekeza zoezi hili lifanyike haraka na kwa umakini mkubwa.

“Ndugu viongozi, kuna hoja ya kufanya rebranding ili kuongeza ufanisi na tija katika kutekeleza adhima hiyo haihitaji fedha, bali mabadiliko ya mtazamo na fikra kwa viongozi, hivyo ni matarajio kuona ubunifu mwingi kutoka miongoni mwenu,”alifafanua kwa kina Katibu Mkuu Kiongozi.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi,Mheshimiwa Balozi Dkt.Kusiluka amebainisha kuwa, kwa upande wa mashirika yanayofanya biashara Serikali inapenda kuona yanatengeneza faida kubwa.

“Tujifunze kwa taasisi za Serikali ambazo Serikali ina hisa ndogo mfano NMB, CRDB ukiona wanavyofanya unajiuliza TCB, TIDB, TIB wanafanya nini?.

“Tujipange vizuri mwakani tuanze kuripoti matokeo ya ‘trend’ nzuri, jengeni mahusiano bora miongoni mwenu na muepukane na migogoro na migongano miongoni mwenu.

“Tumekuwa na taasisi ambazo zinashindana zote zinategemea resources za Serikali, wote wanajipanga kwenda kwa PST kuomba fedha kuanzisha programu ambazo zinafanana, lakini zina ubora mdogo.

“Tunapendana kuona zaidi ushirikiano badala ya mashindano ambayo hayana tija kabisa. Unakuta kwenye vyuo vikuu programu inaanzishwa mfano chuo au hospitali na pia chuo kingine kinapambama kutafuta hospitali wakati ipo nje tu ya chuo kingine, lakini hawashirikiani kila mtu anataka awe na chake.

“TR liangalie jambo hilo lengo ni kupata tija katika taasisi za serikali na mashirika ya umma na wananchi wetu wapate huduma bora na stahiki.

“Pia,viongozi niwatake mshiriki katika mchakato wa hesabu na ukaguzi wa mashirika yenu mutoe ushirikiano kwa CAG,mshiriki pia kujibu hoja kwa wakati msiwaachie watu wa chini.

“Mjiandae pia vizuri mnapokutana na Kamati za Bunge mtoe maelezo ya taasisi zenu na jinsi zilivyo, mafunzo yafanyike kabla ya bodi mpya kuanza kutekeleza majukumu yake hili litakuwa ni la lazima.

“Msajili ubainishe maeneo muhimu yanayohitaji mafunzo sambamba na kuwa na utaratibu wa na tabia ya kusoma sheria, taratibu na miongozo ili muweze kupata uelewa mzuri.

“Imekuwa ni jambo la kawaida Mjumbe wa Bodi kushiriki kikao bila kusoma nyaraka na makaburasha endapo hujasoma tambua mchango wako hauwezi kuwa mzuri.

“Pia mipango na maamuzi yenu naombeni mtumie takwimu sahihi na rasmi za Serikali hasa za sensa ambazo zimechambuliwa vizuri kabisa na kuainishwa vyema.

“Na mwisho nisisitize maazimio ya kikao kazi hiki tuyapate mapema, tuyaone yawezekana tukafanya maboresho baada ya mazungumzo haya mwakani tutakuja kupimwa,”alifafanua na kusisitiza kwa kina

Mheshimiwa Balozi Dkt.Kusiluka.