Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 kama ilivyorekebishwa, Ofisi imepewa majukumu yafuatayo: –
- Kufanya mapitio ya kudumu ama kuhakikisha kunafanyika mapitio ya kudumu ya shughuli na mwenendo wa watu ama Taasisi ambazo Msajili wa Hazina anamiliki mali ama ana maslahi kwa mujibu wa Sheria.
- Bila kuathiri Kifungu kidogo cha (1) kwa ujumla wake, Msajili wa Hazina anatakiwa:
- Kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu uanzishaji wa Mashirika ya Umma na kusimamia biashara au mali zilizowekezwa kwenye Mashirika hayo;
- Kupitia utendaji wa kifedha wa Mashirika kwa lengo la kushauri hatua za kuchukua katika kuunganisha, kuboresha muundo, kufuta au kuboresha utendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma;
- Kuweka malengo ya kifedha na vigezo vingine vya utendaji vitakavyotumiwa na Mashirika na Taasisi za Umma;
- Kufanya tathmini mara kwa mara ili kupima utendaji wa Bodi au Menejimenti za Mashirika na kutoa mapendekezo kwa Serikali ya hatua za haraka au zilizopo za kuboresha usimamizi wa rasilimali;
- Kuidhinisha uwekezaji wa hisa unaofanywa na Mashirika ya Umma kwenye Mashirika au Kampuni nyingine;
- Kuwekeza au kuuza mali za Mashirika ya Umma;
- Kuhakikisha kuwa kila Shirika la Umma linaingia Mkataba wa Utendaji na Msajili wa Hazina mara moja baada ya kuteuliwa kwa Bodi ya Wakurugenzi;
- Kufuatilia na kutathmini programu za mafunzo katika Mashirika na Taasisi za Umma;
- Kuelekeza au kuidhinisha matumizi au marekebisho ya kanuni za fedha ili kuhakikisha usahihi wa taarifa za mapato na matumizi ya Mashirika ya Umma;
- Kuchambua na kuidhinisha Miundo na Mifumo ya Mishahara, Kanuni za Utumishi na Mpango wa Motisha kwa Mashirika na Taasisi za Umma;
- Kufuatilia misaada, ruzuku, fedha za mtaji, akiba au malimbikizo ya faida katika Mashirika ya Umma na kwenye uwekezaji mwingine wa Umma;
- Kupendekeza au kuidhinisha Mipango ya Mwaka ya Mashirika na Taasisi za Umma;
- Kufuatilia na kutathmini utendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma; na
- Kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha gawio, michango na mikopo kutoka katika Mashirika na Taasisi za Umma inalipwa kwa wakati.
Majukumu mengine ya Msajili wa Hazina yameelezwa kwenye Sheria nyingine kama vile Sheria ya Mashirika ya Umma, Sura 257, Sheria ya Bajeti, Sheria ya National Bank of Commerce (Reorganisation and Vesting of Assets and Liabilities) Act, Sura 404 na Sheria ya Fedha.