KUMEKUCHA! Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema ndani ya mwaka mmoja au miwili ijayo, mashirika ya umma yatafanyiwa mabadiliko makubwa yakiwemo ya kuhakikisha yanajiendesha kibiashara.

Pia, ameeleza kuwa yuko katika hatua za mwisho za kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufanyia uchambuzi mashirika hayo, kuyaboresha yale yanayofanya vibaya na kuyaondoa yaliyopitwa na wakati.

Mchechu anayeiongoza ofisi hiyo inayosimamia mali na uwekezaji wote wa Serikali kupitia taasisi takribani 300 katika Taasisi na Mashirika ya Umma kwa niaba ya Rais wa nchi, aliyasema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano baina yake na wahariri wa habari uliokuwa mahsusi kupokea taarifa ya utendaji ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), jana.

Alisema moja ya malengo ya mabadiliko hayo ni kuhakikisha mashirika hayo yanatoa gawio serikalini linafikia asilimia 10 ya bajeti ya serikali kwa sasa yanachangia asilimia tatu tu. Kwa sasa, uwekezaji wote wa Serikali katika Taasisi na Mashirika ya Umma ni Zaidi ya Shilingi Trilioni 70.

Alisema kwa sasa ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika takribani 300 na kati ya hayo 248 inayamiliki asilimia 100 ambayo mpango wake ni kuyasimamia kwa jicho la biashara kwa niaba ya serikali.

“Tunataka mashirika haya yafanye vizuri kama ambavyo sekta binafsi inafanya. Tunataka TTCL ifanye vizuri kama Vodacom. Hakuna sababu mashirika haya yategemee ruzuku huu sio wajibu wetu lazima yajiendeshe bna yatoe mchango wake serikalini,” alisema Mchechu.

Alisema katika mabadiliko hayo kutakuwa na mashirika ambayo yatapimwa, yatapewa malengo, yatapewa malengo, na kuhakikisha yanakuwa na viongozi sahihi wa kuongoza mashirika hayo na kuachiwa uhuru wenye uwajibikaji.

Pia, alisema watayawezesha kirasilimali lengo ni kuongeza mchango wa mashirika hayo katika Pato la Taifa.

“Na hizi taasisi zinachangia non tax revenue yaani pesa isiyokuwa kodi au gawio la mwisho. Lengo letu gawio angalau lifikie asilimia 10 ya bajeti yetu kwa sasa tuko asilimia tatu hadi nne. Na baadae tutaenda hadi asilimia 20 kadri tutakavyoweza,” alieleza.

Alisema Rais Samia anataka kuona mabadiliko na kwa msaada na maagizo aliyotoa hadharani mabadiliko yatafanyika.

Mchechu alisema kuna taasisi ambazo mabadiliko yake yataonekana ndani ya miaka miwili na nyingine hadi  zifumuliwe zikawe vizuri itachukua miaka mitano.

Kuhusu agizo la Rais Samia la kuchambua mashirika hayo alisema liko katika hatua za mwisho ambapo kuna mashirika ambazo majukumu yake yanaingiliana au yanajirudia zitaunganishwa.

Alisema pia yapo mashirika ambayo ni muhimu sana lakini zimekuwa zikifanya vibaya zitawekwa kwenye uangalizi  maalumu na zile zilizopitwa na wakati na hazifanyi vizuri zitaenda kufungwa.

“Zile zinazoyumbayumba bado zina mahitaji tutaziboresha tutazifanyia reforms. Tutawasaidia wale mameneja waliopo  wasiposaidika tutafuta wengine kwa sababu saa nyingine taasisi haina shida, ila shida ni uongozi,” alisema.

Aidha, Mchechu alisema katikankuhakikisha mashirika hayo yanaweka wazi utendaji wake kwa jamii, anatarajia kuweka mkakati wa kuyakutanisha na wahariri wa vyombo vya habari angalau mara mbili kwa wiki.

Alisema imezoeleka mashirika hayo kusikika kwa mabaya kupitia taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huku taarifa za kile kizuri kinachofanywa na mashirika kikiwa hakisikiki.

“CAG ndio kazi yake kufanya ukaguzi na kuibua udhaifu na mabaya yote. Lakini pia sisi tunaweza tukazungumzia mazuri tunayoyafanya ili yasikike. Ndio maana tumeamua kuanzia sasa kila taasisi itakuwa lazima kuweka wazi taarifa zake za hesabu ili kila mtu ajue kinachoendelea,” alieleza.

Alisema wakati CAG anafanya kazi yake ni wakati wa mashirika hayo kujieleza kazi zao ili watanzania wazijue pia.

Alisema anatarajia kukutana na wahariri wa vyombo vya habari Agosti, mwaka huu ili kuweka mkakati mzuri wa kuyakutanisha mashirika hayo na wahariri hao.

Mwisho