Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 

WAKATI Kampuni ya Mawasiliano ya simu ya Airtel Tanzania Plc ikiikabidhi Serikali Sh bilioni 143 kama gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amezitaka taasisi binafsi ambazo Serikali imewekeza hisa hata kama ni asilimia moja kuhakikisha zinajiendesha kwa ufanisi na kulipa gawio stahiki serikalini.

 

Aidha, amezitaka taasisi zisizotoa gawio kujitathmini kwa kuwa serikali iliwekeza ili faida itumike kwa maendeleo ya wananchi.

 

“Taasisi ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo bado zinajiendesha kwa faida, lakini hazitoi gawio stahiki zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa gawio serikalini,” alisema Dk Mpango.

 

Dk Mpango alitoa maagizo hayo wakati akipokea hundi ya Sh bilioni 143 iliyotolewa na Airtel Tanzania Plc kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni gawio, mchango wa uwezeshaji na mauzo ya minara. Airtel Tanzania inamiliki asilimia 51 ya hisa zote wakati Serikali ni mmiliki kwa asilimia 49.

 

Kampuni hiyo kubwa ya pili kwa umiliki wa soko la mawasiliano ya simu nchini, imesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh bilioni 88 ni gawio, Sh bilioni 12 mchango wa uwezeshaji (Support Services Agreement (SSA) na Sh bilioni 43 ni kutokana na mauzo ya minara ya mawasiliano ya Airtel kwenda kwa Minara Tanzania Limited.

 

Akikabidhi hundi  hiyo ya mfano kwa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi  Airtel Tanzania Plc , Gabriel Malata kiasi cha Sh bilioni 88 ambacho Serikali imelipwa kimeweka rekodi ya kuwa kiasi cha juu kulipwa kama gawio kwa makampuni ambayo Serikali inamiliki hisa.

 

“Tunapongeza juhudi za Serikali za kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mfumo wa ubia, ambapo leo hii tunashuhudia mafanikio mazuri ya Airtel Tanzania ” alisema Malata.

 

Alisema kwa miaka mitatu sasa, Airtel Tanzania Plc imeweza kulipa Serikali ya Tanzania zaidi ya Sh bilioni 200 zinazotokana na gawio, mchango wa uwezeshaji wa huduma pamoja na malipo mbalimbali. Pia, imeweza kulipa ada na tozo zilizowekwa kwa mujibu wa sheria jumla ya Sh Bilioni 97 kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

 

Akizungumzia maendeleo ya kampuni hiyo, Malata alisema; “Ninayo furaha kukufahamisha kuwa Airtel Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwenye kuunga mkono juhudi mbalimbali za serikali kulingana na hali ya biashara yetu. Kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 Airtel imetoa fursa za ajira zaidi ya 350,000, kati ya hizi zipo ajira za moja kwa moja na zile ambazo sio za moja kwa moja. Nia yetu ni kuendelea kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa manufaa ya Watanzania.”

 

Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio chanya ya kampuni hiyo kufikia kiasi cha kulipa serikalini gawio la Sh bilioni 143.

 

“Airtel tunaamini kwamba kutokana na Serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji, wawekezaji wazawa na wale wa kutoka nje wataendelea kushirikiana na serikali kama ilivyo kwa Airtel sasa.” alisema Malata.

 

Pia alitoa shukrani kwa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Tume ya Ushindani (FCC), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa mafanikio  yote.

 

Makamu wa Rais, Dk Mpango ambaye alimwakilisha  Rais Samia Suluhu Hassan  alisema Serikali  itaendelea kuweka mazingira mazuri na endelevu ya kufanya biashara.

 

Aidha, Dk Mpango alimpongeza Msajili wa Hazina  kwa kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yanayowezesha kupatikana kwa fedha na  Airtel kuendelea kulipa shilingi bilioni moja kila mwezi.

 

“Tukio hili la leo linaashiria uwepo wa mazingira mazuri ya kiutendaji na mahusiano thabiti ya kibiashara baina ya wabia.  Mapato haya yaliyopatikana yana faida kubwa sana katika kuchangia miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa Watanzania wote. Niwasihi tena tuendeleze jitihada hizi ambazo ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi yetu na manufaa kwa kila mwananchi.” alisema Dk Mpango.

 

Hata hivyo, alitaka kampuni hiyo kujiimarisha na kuendelea kutoa mchango wake kwa manufaa ya taifa na wananchi.

 

“Hii ni siku nzuri sana kwangu ninaposikia taasisi ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache zinafanya vizuri na kulipa gawio (tena kubwa) kwa serikali kutokana na uwekezaji