Na Mwandishi Maalumu

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi rasmi msitu wa Iyembela uliopo mkoani Njombe kwa Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTIDA) baada ya kumaliza mgogoro uliokuwa umeikumba msitu huo kwa muda mrefu na kuvuruga maslahi ya taifa.

Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto alikabidhi kwa niaba ya Serikali wakati Mkurugenzi wa TSHTIDA, Theophold Ndunguru alipokea kwa niaba ya Wakala wa Wakulima wadogo wa chai. Viongozi na maofisa kadhaa akiwemo Mbunge wa Jimbo la Lupembe mkoani Njombe, Edwin Swale na Ponziano Lusasi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali walishuhudia makabidhiano hayo.

Akikabidhi msitu huo unaokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari zaidi ya 1,000, Benedicto alisema anaamini kuwa pamoja na matumizi mengine ambayo yatatekelezwa na TSHTIDA, matumizi ya kwanza na ya msingi ya msitu huo ni kuhakikisha unaendelea kuwa chanzo cha nishati ya kuni kwa ajili ya kukaushia chai kwa Kiwanda cha Chai cha Lupembe pamoja na viwanda vingine ambavyo vinaweza kuanzishwa katika ukanda huo.

“TSHTIDA mhakikishe mnajielekeza katika kusimamia mpango kazi ambao mmeuandaa kwa ajili ya kuhakikisha msitu unahifadhiwa vizuri, unaendelezwa, na kujengewa miundo mbinu yote muhimu kama vile njia za kuzuia moto na kuhakikisha kwamba barabara kwa ajili ya kuingia na kutoka katika shamba la miti zinapitika wakati wote,” alisema Msajili.

Aidha, wameelekezwa kuweka mpango na utaratibu mzuri wa upandaji na uvunaji wa mazao ya misitu ili kuhakikisha shamba linajitosheleza kwa uzalishaji wa kuni na mazao mengine ya misitu na pia linajiendesha kwa faida na kuleta tija kwa Serikali na wakazi wanaozunguka shamba hilo.

Msitu wa Iyembela ni shamba la miti lililopo Kijiji cha Iyembela Kata ya Matembwe, Tarafa ya Lupembe, Mkoani Njombe na limekuwa katika mgogoro baina ya Muungano wa vyama vya Ushirika Lupembe (LFCJEL) na Mwekezaji katika Kiwanda cha Chai Lupembe, kampuni ya Dhow Mercantile East Africa.

Kukabidhiwa kwa msitu huo kwa wakala baada ya kumalizika kwa mgogoro, kumetokana na kubainika kwamba msitu huo haujawahi kuondoka serikalini na kwamba pande zilizojiingiza katika mgogoro hazina nyaraka za uthibitisho wa umiliki halali.

Awali, Serikali ilizikutanisha pande zenye mgogoro ambapo ziliafikiana na kusaini hati ya maafikiano ya kusuluhisha migogoro hiyo (Deed of Settlement) ambayo iliwasilishwa na kusajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Septemba 23, 2021.

Aidha katika Hati ya Maafikiano, moja ya makubaliano ilikuwa ni kushughulikia suala la umiliki wa msitu wa Iyembela.

Baada ya kuwapo kwa maelekezo hayo, Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo inashughulikia maslahi katika mali za serikali iliunda kamati kwa ajili ya kubainisha mmiliki wa Msitu wa Iyembela.

Kamati hiyo ilijumuisha wadau mbalimbali wakiwemo wajumbe kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bodi ya Chai Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai, Lupembe Farmers’ Co-operative Joint Enterprises Ltd (LFCJEL), Dhow Mercantile (EA) Ltd na Ofisi ya Mbunge wa Lupembe.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwanasheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaizilege Kajuna ilitembelea na kufanya tathmini ya Msitu ulivyo, pamoja na kufanya vikao na wadau na kuchambua nyaraka mbalimbali ili kupata mmiliki halali wa msitu huo. Pande zilizokuwa zinavutana hazikuweza kuthibitisha juu ya umiliki wa msitu, hivyo msitu ukatakiwa kubaki kuwa wa Serikali.

Aidha, kamati ilipendekeza msitu huo sasa ukabidhiwe kwa TSHTIDA kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kiwanda kubinafsishwa ili kuutunza na kupangiwa matumizi bora kama ilivyokusudiwa wakati wa uanzishwaji wake.

 

Mwisho