*Yaja na mageuzi makubwa kuifanya benki imara, ya mfano

*Yawahakikishia wateja usalama wa amana zao, huduma bora

 

Na Mwandishi Maalumu, OMH- Dodoma

SERIKALI imetangaza rasmi kuziunganisha Benki ya TPB na TIB Corporate kuanzia Juni Mosi, 2020 kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazomiliki ili kuwa na Benki moja ya biashara ambayo ni imara.

Katika hatua za awali za uamuzi huo, imefafanua kuwa, Benki ya TPB itachukua mali na madeni yote ya TIB kuanzia Juni Mosi, huku ikiwahakikishia wateja usalama wa amana zao na kwamba kwa sasa wataendelea kupata huduma bora katika matawi ya benki zao za awali.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 10 (2) (b) cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura ya 370, ninatangaza kuunganishwa kwa Benki ya TPB (TPB Bank Plc) na TIB Corporate (TIB Corporate Bank Limited) kuanzia leo tarehe 1 Juni, 2020.”

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, katika Mkutano na Waandishi wa Habari.

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, akisisitiza jambo alipokuwa anafafanua jambo kwa waandishi wa habari waliotaka kujua endapo kutakuwa na athari zozote kwa wateja wa Benki ya TIB na TPB kutokana na kuunganishwa kwa benki hizo. Alitangaza kuunganishwa kwa benki hizo mjini Dodoma huku akisisitiza kuwa, hakuna mteja au mfanyakazi yeyote wa benki hizo atakayeathirika kutokana na uamuzi huo wa Serikali.

Alisema muungano wa Benki hizo unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji, kimfumo, kimuundo na taswira ili benki hiyo iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha.

“Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa Benki na taasisi za fedha,” alieleza Mbuttuka

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka (katikati) akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa anatangaza uamuzi wa Serikali wa kuziunganisha Benki za TPB na TIB Corporate jijini Dodoma.

Alisema kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate na Wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.

Aidha, alisema Serikali inawahakikishia wateja wa benki hizo mbili pamoja na umma kuwa huduma za kibenki hazitaathirika kwa vyovyote vile kutokana na mabadiliko hayo.

Uamuzi wa kuziunganisha benki umekuwa sehemu ya mwendelezo wa Serikali  wa kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka (wa tatu kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi, wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wengine baada ya kutangazwa kuunganishwa kwa Benki ya TIB na TPB Corporate, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dodoma.

Kutokana na muunganiko huo, benki ya TPB sasa itaimarika zaidi kimtaji, kwani itakuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni moja kutoka mali za Sh trilioni 657 na itanona zaidi katika amana, kani sasa inakuwa na amana zaidi ya Sh bilioni 700 kutoka Sh bilioni 449.

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka (kulia), akizungumza jambo baada ya kutangaza kuunganishwa kwa Benki ya TIB na TPB Corporate katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dodoma.

Hii si mara ya kwanza kwa Serikali kuchukua hatua katika benki zake, kwani iliwahi kuziunganisha benki za TPB na Twiga Bancorp na baadaye iliiunganisha pia Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), lengo likiwa kuleta ufanisi, matunda ambayo yalionekana katika utendaji wa TPB.

 

Mwisho.