Na Mwandishi Wetu,
UWEKEZAJI wa Serikali katika kampuni mbalimbali, umeiwezesha kupata gawio la Shilingi Bilioni 6.1 kutoka kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited.
Gawio hilo la Serikali yenye umiliki wa asilimia 50 katika Puma Energy, limepokelewa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu katika hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Akipokea gawio hilo, Mchechu ambaye ofisi yake inasimamia uwekezaji wote wa Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitumia fursa hiyo kuipongeza Puma Energy kwa kushirikiana vyema na Serikali kibiashara.

Alisema ushirikiano baina ya pande hizo unaonesha jinsi Serikali inavyoweza kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi, kwani faida ziko wazi na zinanufaisha pande zote mbili.
Pamoja na pongezi, Mchechu ameitaka Bodi na Menejimenti ya Puma Energy Tanzania kuendelea kuwa wabunifu wa huduma mbalimbali na kuona umuhimu wa kupanua shughuli zake nje ya Jiji la Dar es Salaam, akibainisha kuzidi kuwepo fursa kutokana na ukuaji wa kasi wa miji mbalimbali.
Aliipongeza pia kampuni hiyo kwa jitihada za kuwekeza katika nishati mbadala hususani zilizoanzishwa hivi karibuni kama vile huduma za gesi ya LPG, matumizi ya nishati ya jua, na CNG.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah alimweleza Msajili wa Hazina kuwa, Kampuni yake imeanza kuonesha mwelekeo wa kufanya vizuri baada ya athari za kibiashara zilizosababishwa na COVID-19 na faida halisi kwa mwaka ulioishia Desemba 2022 iliongezeka kwa asilimia 11,750 kutoka 2021.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, gawio lililotolewa kwa Serikali limetokana na sehemu ya faida ya Shilingi Bilioni 24.4 kwa mwaka ulioishia Desemba 2022 na hivyo katika kutekeleza Sera ya Gawio, wanahisa wamepata jumla ya Shilingi bilioni 12.21, kiasi cha Shilingi builioni 6.1 kwa Serikali ya Tanzania na kiasi kama hicho kwa Kampuni ya Puma Energy.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Puma Energy kanda ya Afrika, Fadi Mitri amesema Hundi za gawio zilizotolewa zinadhihirisha mchango chanya wa ushirikiano kati ya Puma Energy na Serikali ya Tanzania katika kusaidia ukuaji wa uchumi.

“Kuimarika kwa utendaji wa kampuni pia kunaiwezesha Puma Energy Tanzania kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, huku pia ikisaidia jamii ya Tanzania,” alisema.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&