*Dkt. Philip Mpango asisitiza zinakwenda kuchochea miradi ya maendeleo

 

Na Mwandishi Maalumu

SERIKALI imepokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 15.2 kutoka Benki ya NMB, ikiwa ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 48 iliyopatikana kwa mwaka 2019, hivyo kuifanya iendelee kunufaika na uwekezaji wake katika mashirika ya umma, taasisi na makampuni yake ambamo imewekeza hisa zake.

Makabidhiano ya mfano wa hundi za gawio hilo yalifanyika Jijini Dodoma kati ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Dkt. Edwin Mhede na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliyepokea gawio hilo kwa niaba ya Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mpango, alisema Serikali inathamini mchango wa Benki ya NMB katika maendeleo ya nchi na kuupongeza uongozi wa Benki hiyo kwa jitihada mbalimbali za kuchangia uchumi wa nchi ikiwemo kutoa gawio ambalo mwaka huu limeongezeka.

Katika mwaka wa Fedha 2018/19, Benki ya NMB ilitoa gawio la shilingi bilioni 10.48 na mwaka huu imetoa shilingi bilioni 15.2, sawa na ongezeko la asilimia 45.

“Ni mafaniko makubwa kwani faida imepatikana wakati wa changamoto ya ugonjwa wa Covid 19; NMB ni ya mfano katika sekta ya fedha hapa nchini”, alisema Dkt. Mpango.

Waziri Dkt. Mpango aliahidi kuwa Wizara yake itahakikisha fedha hizo zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutatua baadhi ya kero za wananchi na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Doto James kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Aidha, Waziri Dkt. Mpango ameiagiza Benki ya NMB pamoja na taasisi zingine za fedha nchini kutumia utaalamu kutafuta suluhisho la riba kubwa ili amana na mikopo kwa wananchi iongezeke.

“Benki zijitahidi kujua uchumi wa maeneo mbalimbali na kuandaa namna ya kuwafikia wateja katika maeneo yao ya biashara, kuwapatia elimu ya fedha, na kusimamia vizuri kanuni za utoaji mikopo”, alisisitiza Dkt. Mpango.

Alizitaka benki na taasisi zote za fedha nchini kushughulikia mikopo chechefu ili uwiano wa mikopo yote isivuke asilimia tano na kuhakikisha wananchi, hususani wakulima na wananchi wa kipato cha chini, waweze kufikiwa.

Aidha, Waziri Dkt. Mpango alitumia fursa hiyo kumpongeza Msajilli wa Hazina, Ndg. Athumani Mbuttuka kwa usimamizi makini wa mashirika ya umma, taasisi, na makampuni ambayo Serikali ina hisa hivyo kuiwezesha Serikali kupata gawio kulingana na uwekezaji.

Waziri Dkt. Mpango amewapongeza wanahisa wengine wa Benki ya NMB hususani Rabo Bank ya Uholanzi kwa kuwa wabia wazuri na kuwa Serikali inathamini mchango wao katika maendeleo ya Benki ya NMB na itaendelea kushirikiana nao.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Ndg. Athumani Mbuttuka alifafanua kuwa mchango wa mashirika ya umma, taasisi, pamoja na makampuni umeongezeka ambapo gawio la Serikali limeongezeka ndani ya miaka mitano. Akifafanua zaidi, Ndg. Mbuttuka alisema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2014/15 Serikali ilipata gawio la shilingi bilioni 161, ambapo kwa sasa gawio limepaa na kufikia shilingi trilioni 1.05 katika Mwaka wa Fedha 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 521.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede alieleza kuwa Benki hiyo inatarajia kuongeza kiwango cha gawio kwa Serikali katika mwaka ujao wa fedha wa 2020/21, baada ya Benki hiyo kupata faida ya shilingi bilioni 93.6 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, aliyeteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo, alisema gawio la shilingi bilioni 15.2 linatokana na uwekezaji wa Serikali wa asilimia 31.8 za hisa katika Benki hiyo.

Alisema pamoja na kutoa gawio kwa Serikali, Benki ya NMB imekuwa ikishiriki katika miradi mbalimbali ya kimkakati ya taifa ikiwemo kutoa dhamana katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Umeme wa Kinyerezi II, pamoja na kuchangia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, afya, na kilimo. Aidha, Bi. Ruth Zaipuna aliahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa mchango chanya katika jamii.

Aliongeza kuwa, pamoja na kutoa gawio hilo, benki yake pia imelipa kodi mbalimbali serikalini zikiwemo kodi ya mapato, kodi ya maendeleo ya ujuzi, ushuru wa forodha, na kodi ya ongezeko la thamani zenye thamani ya shilingi bilioni 170.8.

&&&&&&&&&&&&&&&&&