Na Mwandishi Wetu

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu ameendelea kusisitiza umuhimu wa kubadili fikra katika uwekezaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini ili kuhakikisha unakuwa na matokeo chanya na hivyo kuleta tija kwa uchumi wa nchi.

Kutokana na dhamira hiyo, amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu katika taasisi za Serikali kuhakikisha taasisi hizo ambazo kwa ujumla uwekezaji wake unafikia Shilingi Trilioni 70, zinakuwa na matokeo chanya kwa uchumi na maendeleo ya taifa.

Aliyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Miaka 25 ya Benki ya NMB mwishoni mwa wiki ambayo yalikwenda sambamba na utoaji wa gawio kwa Serikali la kiasi cha Shilingi bilioni 45.5.

Akizungumza katika hafla hiyo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mchechu amemtaja Rais huyo kuwa ni kinara wa mageuzi ya kidemokrasia na uchumi, hivyo taasisi za Serikali pia zinapaswa kuwa na mtazamo huo.

“Siku zote mabadiliko ya uchumi yanakuwa na mtazamo tofauti na vikwazo vingi. NMB ni hadithi nzuri tunaishi leo ikituonyesha tulikotoka. Wakati NMB inakwenda kwenye awamu ya pili ya ubinafsishaji wengi walipinga ikiwemo bodi na ilibidi Rais amtoe Mwenyekiti na bodi ivunjwe ili mchakato uendelee.

“Hadi dakika hii tuna benki ambazo zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, ukienda kwenye bajeti iliyosomwa juzi tumeweka lengo la kuzipa mtaji hizo benki na mimi katika Ofisi ya Msajili wa Hazina sijapokea hata senti ya rejesho. Sasa tujiulize, jema ni lipi? Tumiliki asilimia 100 halafu tuendelee kutoa kwenye chungu kuwapa hao au tukaenda katika mfumo huu wa NMB,” alisema na kusisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuziona taasisi zake zinakua hivyo amewataka wenyeviti wa bosi na maofisa watendaji wakuu kukaa tayari kufanikisha lengo hilo.

“Haya tunayoyaona kwa NMB tunataka kuyaona kwenye taasisi zote hivyo wenyeviti na watendaji wakuu wajiandae vizuri. Ndiyo maana tunaposema unapofanya mageuzi na wewe (Rais Samia) umekuwa Rais wa mageuzi ya kiuchumi na kidemokrasia wapo wanaokuelewa na wasiokuelewa sasa watakuelewa baadaye,” alisema Mchechu.

Mwito wa Msajili wa Hazina ulipewa uzito Zaidi na Rais Samia baada ya kuyataka mashirika yote ya umma kujiendesha kwa ufanisi, tija na ushindani ili yaweze kuwa endelevu.

Rais Samia, akipokea gawio la NMB, alisema Serikali inaendelea kufanya tathmini ya utendaji wa mashirika yote ya umma na yale ambayo Serikali ina hisa kubwa ili kubaini mashirika yasiyo na faida yanayoshindwa kujiendesha na kuitia hasara Serikali.

Alisema tathmini hiyo inafanywa na Msajili wa Hazina ambapo Serikali itayachukulia hatua na kuyafuta mashirika ambayo hayafanyi vizuri, kuyasaidia na kuyapa miongozo ya namna ya kujiendesha ili yapate faida.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&