*Zatoa trilioni 1/-, ni ongezeko la asilimia 552

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, mapato yanayotokana na gawio na michango yanayotokana na kampuni, taasisi na mashirika yameongezeka kwa asilimia 552, kutoka Sh bilioni 161.04 mwaka 2014/15 hadi kufikia Sh trilioni 1.05 katika mwaka wa fedha 2018/19.

Hayo yalianikwa hivi karibuni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango jijini Dodoma wakati wa hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki Ikulu ya Chamwino, Dodoma ambako kampuni na taasisi za umma zilikuwa zinawasilisha michango na gawio serikalini mbele ya Rais, Dk John Magufuli.

“Mapato hayo ya mwaka 2018/19 yanajumuisha mapato yaliyokusanywa kupitia akaunti zilizopo chini ya Msajili wa Hazina ambazo zilileta jumla ya bilioni 683.23.

Fedha zilizopelekwa moja kwa moja mfuko mkuu wa serikali kutoka taasisi na Mawakala ya Usimamzi wa Bandari (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha ambapo yote yalitoa kiasi cha Shilingi bilioni 370.59,” alisema Dk Mpango

Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Fedha, katika kipindi cha mwaka 2018/19, makusanyo yanayopita katika akaunti ya msajili wa hazina yamevuka lengo kwa kukusanya bilioni 683.23 ikilinganishwa na malengo ya Sh. Bilioni 597.77, ikiwa ni ongezeko la asilimia 114.3 ya malengo yaliyowekwa.

Akieleza siri ya mafanikio hayo, waziri huyo ambaye kitaaluma ni mchumi amesema, sera na usimamizi bora wa rasilimali za serikali ndani ya mshirika yanayotoa gawio na michango, kuimarisha ufuatiliaji na uchambuzi ni miongoni mwa sababu za ongezeko hilo.