Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Ofisi ya Msajili wa Hazina yakutana na Balozi wa China kuimarisha ushirikiano
18 May, 2026
Ofisi ya Msajili wa Hazina yakutana na Balozi wa China kuimarisha ushirikiano

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, pamoja na ujumbe wake, katika kikao kilicholenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, uwekezaji na mageuzi ya mashirika ya umma.

 

Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam Jumatatu, Mei 18, 2026, kati ya menejimenti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiongozwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, na ujumbe wa Ubalozi wa China ulioongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian.

 

Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili masuala ya uwekezaji wa serikali, usimamizi wa kampuni za umma na miradi ya kimkakati.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mchechu alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu la kusimamia uwekezaji wa serikali katika taasisi na kampuni 308, ambapo 252 kati yake serikali ina hisa nyingi.

 

Alibainisha kuwa thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi na kampuni hizo ni Sh92.3 trilioni.

 

Alisema uwekezaji huo unahusisha sekta mbalimbali zikiwemo usafiri wa anga, nishati, mafuta na gesi na madini, akisisitiza kuwa serikali inaendelea na mwelekeo wa kuongeza ufanisi na uhimilivu wa kifedha katika mashirika hayo.

 

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema China itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta za uwekezaji, miundombinu na mageuzi ya kiuchumi, akibainisha kuwa uhusiano wa nchi hizo mbili umejengwa katika msingi imara wa miaka mingi ya urafiki na imani ya kisiasa.

 

Balozi Chen aliongeza kuwa China itaendelea kusaidia jitihada za Tanzania katika kuendeleza viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali za madini, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika mafunzo na uhamishaji wa teknolojia kwa watumishi wa umma.

 

Aidha, alieleza kuwa China itaendelea kuunga mkono miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo sekta ya usafirishaji, nishati na uwekezaji wa pamoja katika kampuni za kimkakati.