Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Msajili wa Hazina azindua Mpango Mkakati wa NMB 2026–2030
28 Jan, 2026
Msajili wa Hazina azindua Mpango Mkakati wa NMB 2026–2030

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, siku ya Jumatano, Januari 28, 2026, alizindua Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa Benki ya NMB wa mwaka 2026 hadi 2030 (Agenda 2030).

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo unaolenga kuboresha utendaji kazi wa benki hiyo, Bw. Mchechu aliupongeza uongozi wa NMB na Bodi ya Wakurugenzi kwa kuifanya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki bora zinazochangia kwa kasi ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

 

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Serikali, inayomiliki asilimia 31.8 ya hisa za NMB, imepata Sh670 bilioni kutokana na uwekezaji wake katika benki hiyo, ambapo kati ya kiasi hicho, Sh224 bilioni ni gawio.

 

Sanjari na hilo, aliipongeza Benki ya NMB kwa kuoanisha vipaumbele vyake na maono ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, hususani katika maeneo ya afya, elimu, ujasiriamali na mazingira.

 

Katika kusisitiza umuhimu wa mwelekeo huo wa maendeleo, Bw. Mchechu alisema anatamani kuona taasisi zote nchini, ikiwemo za sekta binafsi, zikioanisha mikakati yao na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

 

Alitaja Benki ya NMB kuwa mfano wa taasisi inayotekeleza mwelekeo huo kupitia utendaji wake wa kifedha na usimamizi makini wa mikopo.

 

“Benki ambayo imekuwa ikitoa wastani wa mikopo ya Sh5.6 trilioni kwa mwaka halafu inakuwa na wastani wa mikopo chechefu wa asilimia 2.5 ni kitu cha ajabu sana, hongereni sana NMB,” alisema.

 

Aidha, aliwataka wateja na wawekezaji kuendelea kuiamini na kupata huduma kutoka Benki ya NMB, akisisitiza kuwa ni sehemu salama kwa kuwekeza fedha zao.

 

Akizungumza awali wakati wa uzinduzi wa Agenda 2030, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo inajivunia mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikifunga kwa kuvuna faida ya Sh trilioni 1.1, sawa na ongezeko la asilimia 15.

 

Katika mchanganuo wake, Bi. Zaipuna alifafanua kuwa faida baada ya kodi kwa mwaka 2025 ni Sh750 bilioni ambalo ni ongezeko la asilimia 16, huku mapato yote ya taasisi hiyo yakiwa ni Sh1.82 trilioni (ongezeko la asilimia 11) na mali zote za benki zikiwa na thamani ya Sh17.2 trilioni.

 

“Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa MTP 2025, NMB imepata matokeo madhubuti, yaliyojumuisha utendaji imara wa kifedha na mchango mpana katika kuchochea na kuwezesha shughuli za kiuchumi,” alisisitiza Bi Zaipuna.

 

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitano, benki ilizalisha faida ya jumla ya Sh2.7 trilioni.

 

Aidha, mikopo yote iliyotolewa ilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh27.6 trilioni, huku amana za wateja zikifikia Sh12.4 trilioni na idadi ya akaunti za zao ikiongezeka hadi milioni 9.9.

 

Bi. Zaipuna alisema benki yake inajivunia mafanikio iliyopata katika MTP 2025, na kwamba ana imani kubwa kwamba MTP 2030 utakuwa kichocheo cha ukuaji bora wa NMB, akiamini unaenda kujenga benki imara yenye ukuaji endelevu wenye kuakisi mahitaji ya soko ya sasa na baadae.

 

Alisema Mpango Mkakati huo mpya umejengwa juu ya mafanikio yaliyopatikana na unaweka dira ya ukuaji endelevu unaoongozwa na mteja, teknolojia na tija ya kiutendaji.

 

Katika kipindi hiki kipya cha kimkakati, benki hiyo itaweka mkazo mahsusi katika kuboresha huduma kwa wateja kwa kiwango cha juu, kuimarisha mabadiliko ya kidijitali pamoja na matumizi ya kimkakati ya data.

 

Aidha, benki hiyo pia imesema itaweka mkazo katika kufadhili sekta za kimkakati zinazochochea ajira, uzalishaji na ongezeko la thamani katika uchumi — zikiwemo kilimo, ujenzi, viwanda, utalii, nishati na madini.

 

“Mpango huu utapanua wigo wa shughuli zetu zaidi ya huduma za sasa za kibenki, sambamba na kupanua uwepo wa benki nje ya mipaka ya Tanzania. Tunakwenda kuwekeza na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa viwango vya juu vya ubora na ufanisi katika masoko ya nje,” alisisitiza.