Msajili wa Hazina na Arise Investments kuimarisha uwekezaji NMB
Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, leo Machi 11, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Gavin Tipper, Afisa Mtendaji Mkuu wa Arise Investments, pamoja na ujumbe wake katika ofisi yake jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujadiliana masuala yanayohusu uwekezaji na ushirikiano katika benki ya NMB Tanzania.
Kampuni ya Arise Investments ni mmoja wa wanahisa wakubwa katika benki ya NMB Tanzania ikiwa na hisa asilimia 34.9, huku Ofisi ya Msajili wa Hazina ikimiliki asilimia 31.8.
Katika mazungumzo yao, Bw. Mchechu aliwashukuru wageni hao kwa kutembelea ofisi yake na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya wanahisa wa benki hiyo.
Aidha, alieleza kuwa wanahisa wanapopata nafasi ya kuteua wajumbe wa bodi, ni muhimu kuhakikisha wanateua wakurugenzi wenye uwezo na uadilifu, watakaofanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya wanahisa wote na ustawi wa taasisi.
“Hatupaswi kuteua wajumbe wa bodi kwa kuzingatia maslahi binafsi au ya taasisi wanazotoka. Tunapaswa kuangalia maslahi mapana ya wanahisa na taasisi,” alisisitiza Bw. Mchechu.
Kuhusu utendaji wa benki ya NMB Tanzania, ilielezwa kuwa benki hiyo inaendelea kufanya vizuri kwa sasa.
Benki ya NMB inajivunia mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikifunga mwaka wa 2025 kwa faida kabla ya kodi ya Sh1.1 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Katika muktadha huu wa mafanikio, pande zote zilikubaliana kuwa ni muhimu kuendelea kuunga mkono menejimenti na wafanyakazi wa benki ili kudumisha na kuendeleza mafanikio hayo.