Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Watumishi Ofisi ya Msajili wa Hazina wapigwa msasa kuhusu ukusanyaji wa taarifa za utafiti
11 May, 2026
Watumishi Ofisi ya Msajili wa Hazina wapigwa msasa kuhusu ukusanyaji wa taarifa za utafiti

Na Mwandishi wa OMH

Dodoma. Watumishi 19 wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) wamehudhuria mafunzo ya siku tatu kuhusu ukusanyaji wa taarifa za utafiti.

 

Mafunzo hayo yameanza leo Mei 11, 2026 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utafiti kuhusu uelewa wa chapa ya OMH ‘OTR Brand Awareness & Stakeholder Satisfaction Survey’.

 

Wakufunzi wa mafunzo hayo na utafiti huo, unaoratibiwa na Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mipango, Utafiti na Maendeleo ya OMH, wanatoka katika kampuni ya HESA Africa Research & Consulting.

 

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano OMH, Bw. Sabato Kosuri, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatawajengea uwezo watumishi katika ukusanyaji sahihi wa taarifa za utafiti kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.

 

Aidha, alisema kuwa utafiti huo ni muhimu kwa kuwa utapima kwa utaratibu kiwango cha uelewa wa wadau, mtazamo wao pamoja na imani waliyonayo kuhusu OMH.

 

“Matokeo ya utafiti yatazalisha takwimu za kitaalamu zitakazosaidia kuongoza maamuzi ya kimkakati katika mawasiliano, ushirikishwaji wa wadau na usimamizi wa taswira ya Ofisi,” alisema Bw. Kosuri.

 

Vilevile, aliongeza kuwa matokeo hayo yatasaidia kuboresha mkakati wa chapa, ujumbe wa taasisi na namna ya utoaji huduma ili kuhakikisha vinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa pamoja na matarajio ya umma.