Mchechu: Masoko ya mitaji kufungua fursa za uchumi wa Afrika
Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano na ujumuishaji wa masoko ya mitaji, akisema kuwa masoko imara na yaliyounganishwa ndiyo msingi wa kuhamasisha uwekezaji wa muda mrefu, kugharamia miradi ya maendeleo na kuharakisha mageuzi ya uchumi wa bara hilo.
Akizungumza wakati wa kufunga Jukwaa la 13 la Kuendeleza Masoko ya Fedha ya Afrika (BAFM 2026) lililofanyika jijini Dar es Salaam, Bw. Mchechu alisema Afrika ina taasisi imara, rasilimali za kutosha na wataalamu wenye uwezo wa kujenga masoko ya mitaji yenye ushindani wa kimataifa.
Alisisitiza kuwa kufanikisha azma hiyo kunahitaji kuimarisha ushirikiano na ujumuishaji wa masoko ya mitaji barani Afrika.
Alisema kongamano hilo la siku mbili, lililowakutanisha washiriki zaidi ya 150 kutoka masoko ya hisa 18 barani Afrika na kwingineko duniani, limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano na kutafuta suluhisho za pamoja kwa ajili ya maendeleo ya masoko ya mitaji barani Afrika.
Bw. Mchechu alisema kaulimbiu ya kongamano hilo, “Kuchochea Ukuaji wa Masoko ya Mitaji Barani Afrika kupitia Ubunifu, Ujumuishaji na Ushiriki Jumuishi”, imeakisi vipaumbele muhimu vinavyohitajika katika kuimarisha ushindani na ukuaji wa masoko ya mitaji barani Afrika.
Kwa mujibu wa Bw. Mchechu, mada zilizowasilishwa kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali, fedha endelevu, ujumuishaji wa masoko ya mitaji kuvuka mipaka ya nchi, ufadhili wa biashara ndogo na za kati (SMEs), Sukuk, ujumuishi wa kifedha pamoja na ubunifu wa bidhaa za kifedha zimeonesha kuwa Afrika ina uwezo wa kujenga masoko ya mitaji yenye uimara na ushindani wa kimataifa.
Alisema Afrika bado inakabiliwa na pengo la ufadhili wa miundombinu linalozidi dola za Marekani bilioni $100 bilioni kwa mwaka, hali inayofanya uwepo wa masoko ya mitaji yenye ufanisi kuwa hitaji la lazima badala ya chaguo.
"Rasilimali za Serikali na mikopo ya benki za biashara pekee haviwezi kuziba pengo hili,” alisema.
“Masoko ya mitaji yenye nguvu ni muhimu katika kufadhili maendeleo ya viwanda, kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuharakisha mpito wa nishati safi, kuendeleza uchumi wa kidijitali na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda.
Bw. Mchechu alisema kuwa kama Msajili wa Hazina, Ofisi yake inasimamia uwekezaji wa Serikali katika taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache 308, zenye thamani ya Sh92.3 trilioni.
Alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kusimamia uwekezaji huo kwa kuimarisha misingi ya utawala bora, nidhamu ya kifedha, ubora wa utendaji na uendelevu wa thamani ya uwekezaji wa umma.
"Masoko ya mitaji yanatoa fursa muhimu kwa Serikali na Mashirika ya Umma kupata mitaji ya muda mrefu huku yakiongeza uwazi, uwajibikaji, ufanisi wa kiutendaji na imani ya wawekezaji," alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uwazi katika masoko ya fedha, kuhamasisha ubunifu wa kifedha na kupanua ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.
Aidha, alisema utekelezaji wa Dira 2050 utahitaji uwekezaji mkubwa wa muda mrefu katika sekta za miundombinu, viwanda, nishati, kilimo, makazi, elimu na uchumi wa kidijitali, hivyo kuifanya sekta ya masoko ya mitaji kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa.
Bw. Mchechu alizihimiza taasisi za masoko ya hisa barani Afrika kutumia teknolojia zinazoibukia kama Akili Bandia (Artificial Intelligence - AI), blockchain, teknolojia za usimamizi wa mifumo ya udhibiti (RegTech) pamoja na uchambuzi mkubwa wa takwimu ili kuongeza ufanisi wa masoko, kuimarisha ulinzi wa wawekezaji na kupanua ujumuishi wa kifedha.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya masoko ya mitaji ya Afrika kupitia mifumo ya udhibiti inayolingana na miundombinu inayoweza kuunganishwa, hatua itakayoongeza ukwasi, kupunguza gharama za upatikanaji wa mitaji na kupanua fursa za uwekezaji katika bara zima.
"Hakuna soko la mitaji la Afrika linaloweza kufikia uwezo wake kamili likiwa peke yake. Tunapaswa kujenga mfumo wa masoko ya mitaji uliounganishwa barani Afrika, unaowezesha mtaji, taarifa, bidhaa za uwekezaji na wawekezaji kusafiri kwa urahisi kuvuka mipaka ya nchi zetu," alisema.