Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

OTR na TAZAMA zajadili mwelekeo wa biashara
09 Nov, 2026
OTR na TAZAMA zajadili mwelekeo wa biashara

Na Mwandishi wa OTR

 

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) na Kampuni ya Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) zimejadili mwelekeo wa kimkakati wa kampuni hiyo, fursa za kibiashara na umuhimu wa kuimarisha ushindani wake katika soko la usafirishaji wa nishati kikanda.

 

Majadiliano hayo yalifanyika Novemba 9, 2026, wakati OTR ilipompokea Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TAZAMA kutoka Zambia, Ian Mutale, aliyefanya ziara ya utambulisho kwa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, jijini Dar es Salaam.

 

Serikali ya Tanzania, kupitia OTR, inamiliki asilimia 33.3 ya hisa za TAZAMA, huku Serikali ya Zambia ikimiliki asilimia 66.7 zilizobaki.

 

Katika ziara hiyo, Bw. Mutale aliambatana na Mkurugenzi wa Huduma za Kampuni wa TAZAMA, Mussa Mbura, pamoja na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uhandisi, Dora Ernest. 

 

Katika mazungumzo hayo, Bw. Mchechu alisisitiza umuhimu wa kusimamia uwekezaji wa umma kwa kuzingatia mtazamo wa kimkakati wa umiliki wa hisa, unaotanguliza uimara wa biashara, ukuaji wa kampuni na uongezaji wa thamani ya uwekezaji.

 

Alieleza kuwa maamuzi ya kibiashara yanapaswa kuzingatia tija na maslahi ya wanahisa, huku kampuni zikisimamiwa kwa kuzingatia utendaji bora na uendelevu wa muda mrefu.

 

Kwa upande wake, Bw. Mutale alieleza kuhusu nafasi ya kimkakati ya TAZAMA katika soko la kikanda la usafirishaji wa mafuta ya petroli, akigusia maendeleo ya miundombinu ya njia mbadala za usafirishaji na athari zake zinazoweza kujitokeza kwa biashara ya kampuni hiyo siku zijazo.

 

Alitaja Ukanda wa Lobito na njia nyingine mpya za usafirishaji zinazoendelea kujengwa, akibainisha kuwa maendeleo hayo yanabadilisha mazingira ya ushindani katika sekta ambayo TAZAMA inafanya kazi.

 

Aidha, Bw. Mutale alieleza uwezekano wa kupanua shughuli za kibiashara za TAZAMA nchini Tanzania, akitaja miundombinu iliyopo, uwepo wa kampuni nchini na mahusiano yake ya muda mrefu kuwa ni fursa muhimu katika kutafuta maeneo mapya ya kukuza biashara.

 

Alibainisha kuwa Tanzania ni eneo lenye fursa za asili za upanuzi wa biashara ya TAZAMA, kwa kuzingatia kuwa kampuni hiyo tayari ina miundombinu na msingi wa shughuli zake nchini, tofauti na masoko mapya ambako ingehitaji kuwekeza katika kujenga miundombinu na kuanzisha mahusiano mapya ya kibiashara.