OTR yafungua milango kwa RMB kushiriki mageuzi ya taasisi za umma
Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imefungua milango kwa Rand Merchant Bank (RMB) kuangalia fursa za ufadhili na uwekezaji katika taasisi na kampuni za umma zilizo katika usimamizi wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kupata mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati na kupanua shughuli za kiuchumi.
Mwaliko huo ulitolewa Jumanne, Novemba 18, 2026, na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alipokutana na ujumbe wa FirstRand Bank Limited, ambayo huendesha shughuli zake za kibenki na uwekezaji kupitia RMB, ulioongozwa na Bw. John Njuguna, Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wateja wa Taasisi katika Ukanda wa Afrika Mashariki, katika ofisi za OTR jijini Dar es Salaam.
FirstRand Bank Limited ni miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha barani Afrika, ikiwa imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Johannesburg, Afrika Kusini, na Soko la Hisa la Namibia, na thamani ya mtaji wake katika soko la hisa inayozidi dola za Marekani bilioni 30.
Kupitia RMB, benki hiyo ina uzoefu wa muda mrefu wa kutoa suluhisho za ufadhili kwa serikali, kampuni na taasisi zinazomilikiwa na umma, taasisi za kifedha na kampuni za sekta binafsi katika Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania.
Mazungumzo hayo yalihusu fursa za ufadhili na uwekezaji katika sekta za miundombinu, nishati jadidifu, kilimo, usafirishaji, mawasiliano, madini, dawa na maeneo mengine ya uzalishaji, kwa kuangalia namna utaalamu wa kifedha wa RMB unavyoweza kusaidia taasisi na kampuni za umma kupata mitaji ya kutekeleza miradi ya kimkakati na kupanua shughuli zao.
Bw. Mchechu alisema OTR iko tayari kuratibu ushirikiano kati ya benki hiyo na taasisi za umma ili kubaini miradi yenye tija kibiashara na kuandaa mifumo ya ufadhili inayokidhi mahitaji ya kila taasisi.
OTR inasimamia taasisi na kampuni za umma 308, zikiwemo kampuni 252 ambazo Serikali inamiliki hisa nyingi na kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki hisa chache.
Thamani ya jumla ya uwekezaji katika taasisi na kampuni hizo inafikia Sh trilioni 92.3, ikiwa ni mtaji mkubwa wa umma ambao unaweza kutumika zaidi kuchochea shughuli za kiuchumi na ukuaji wa uchumi nchini.
Bw. Mchechu alisema Serikali inazihimiza taasisi za umma kuimarisha uwezo wao wa kujiendesha kifedha kwa kutumia ipasavyo rasilimali na mali walizonazo ili kuvutia mitaji, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa fedha zinazotengwa katika bajeti ya Serikali.
Alieleza kuwa njia mbadala za kupata mitaji ni pamoja na mikopo kutoka benki za biashara, utoaji wa hati fungani na uuzaji wa hisa kupitia soko la mitaji.
Aliihimiza RMB kuchunguza fursa zilizopo katika taasisi hizo na kuandaa mapendekezo ya ufadhili yatakayojadiliwa kwa pamoja na OTR na kampuni husika.
Kwa upande wake, Bw. Njuguna alisema RMB ina nia ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma nchini, ikitumia uzoefu wake katika kufadhili miradi ya miundombinu na shughuli za kibiashara katika masoko mbalimbali ya Afrika.
Alibainisha kuwa vipaumbele vya Tanzania katika maendeleo ya miundombinu, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika biashara na usafirishaji wa kikanda, vinatoa fursa kwa benki hiyo kuchangia kupitia suluhisho za kifedha na uwekezaji zinazolingana na mahitaji ya miradi husika.
Naye Mkuu wa Suluhisho za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu wa RMB kwa Afrika, Bi. Sindisiwe Mosoeu, alieleza kuhusu mifumo mbalimbali ya ufadhili inayoweza kutumika katika miradi ya taasisi za umma.
Mifumo hiyo ni pamoja na ufadhili wa miradi, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, na ufadhili wa miradi ya nishati jadidifu.
Alieleza kuwa aina ya ufadhili inayofaa kwa kila mradi itategemeana na aina ya shughuli zinazotekelezwa, uwezo wa mradi kuzalisha mapato, uwezekano wake wa kujiendesha kibiashara na uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje.
Bi. Mosoeu pia alieleza kuhusu uzoefu wa RMB katika kufadhili miradi ya nishati jadidifu, hususan inayotumia nishati ya jua, upepo na maji katika nchi mbalimbali za Afrika.
Uzoefu huo unaweza kuwa na manufaa kwa taasisi za umma zinazolenga kuendeleza miradi ya nishati na kupanua vyanzo vyao vya mitaji.
Mtaalamu wa Uandaaji wa Miundo ya Uwekezaji katika Masoko ya Kimataifa wa RMB kwa Afrika, Bw. Sinethemba Mvandamba, alisema benki hiyo ina uwezo wa kuwaunganisha wateja wake na vyanzo vya mitaji katika masoko ya kimataifa, hatua inayoweza kupanua wigo wa chaguzi za ufadhili zinazopatikana kwa kampuni na taasisi barani Afrika.