Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

OTR, Rais wa zamani wa AfDB wajadili mageuzi ya mashirika ya umma
22 Sep, 2026
OTR, Rais wa zamani wa AfDB wajadili mageuzi ya mashirika ya umma

Na Mwandishi wa OTR

 

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Jumatatu, Septemba 21, 2026, ilifanya mazungumzo na Dr. Akinwumi Adesina, mwanauchumi mashuhuri wa maendeleo kutoka Nigeria na aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuanzia mwaka 2015 hadi 2025, katika Ofisi za OTR jijini Dar es Salaam.

 

Katika mazungumzo hayo, menejimenti ya OTR, ikiongozwa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ilibadilishana uzoefu na mitazamo na Dkt. Adesina kuhusu mageuzi na maboresho yanayohitajika katika mashirika na taasisi za umma ili kuimarisha ufanisi na mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi.

 

Bw. Mchechu alisema azma yake ni kuona Serikali, kupitia OTR, ikipata mapato makubwa zaidi kutoka katika mashirika ya umma yanayofanya kibiashara kuliko yale yenye majukumu ya udhibiti.

 

Alisema pia shauku yake ni kuona mashirika hayo yakifanya biashara kwa ufanisi, yakipata faida na kulipa gawio kwa uendelevu, ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

 

“Tunataka kuwa na taasisi na mashirika ya umma ambayo yana uwezo wa kujiendesha kibiashara na kifedha. Tunataka kuona mashirika na taasisi za umma zinapunguza utegemezi,” alisema Bw. Mchechu.

 

Kwa upande wake, Dkt. Adesina alisema mageuzi na mabadiliko ya msingi katika mashirika ya umma yanayo fanya biashara ni muhimu ili kubadili mwenendo wa utendaji wao na kuhakikisha yanafanya kazi kwa ufanisi zaidi.

 

Alisema mkazo haupaswi kuwekwa kwenye idadi ya mashirika yanayochangia fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali, bali kwenye kuongeza tija na manufaa ya jumla yatokanayo na uwekezaji wa Serikali katika mashirika hayo.

 

Dkt. Adesina alisema ili OTR iweze kusimamia kwa ufanisi taasisi na mashirika 308 ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, ni muhimu OTR kuwa na rasilimali watu yenye ujuzi, weledi na uwezo mkubwa.

 

Aidha, alisema utendaji wa taasisi na mashirika ya umma yasiyofanya shughuli za kibiashara unapaswa kupimwa kwa kuzingatia ubora wa huduma wanazotoa, kwa kuwa si taasisi zote zinazoweza kutimiza vigezo vya kibiashara.