OTR: Ushirikiano wa wafanyakazi, msingi wa mafanikio kwa taasisi za umma
Na Mwandishi wa OTR
Kibaha, Pwani. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amesema mafanikio ya taasisi za umma hayawezi kupatikana kwa kuweka mkazo kwenye malengo ya kifedha pekee, bali yanahitaji mazingira bora ya kazi, ushirikiano wa wafanyakazi na uongozi unaoweka watu mbele ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji wa kila siku.
Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, Julai 11, 2026, Bw. Mchechu alisema wafanyakazi hutumia sehemu kubwa ya muda wao wa uzalishaji wakiwa kazini, hivyo ni muhimu kujenga mahusiano mazuri yanayowezesha kila mmoja kufanya kazi kwa ari, kujifunza, kushirikiana na kufurahia mazingira ya kazi.
Alionya kuwa mazingira yenye migogoro na mahusiano yasiyo mazuri huathiri afya ya akili, morali ya kazi na hatimaye utendaji wa taasisi.
Alisema mafanikio ambayo OTR imeendelea kuyapata ni matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi wote, akiwapongeza kwa mchango wao katika kuimarisha usimamizi wa uwekezaji wa umma na kuongeza mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali.
Alisisitiza kuwa kila mafanikio yanayopatikana ni ushindi wa timu nzima na si wa mtu mmoja mmoja au idara moja.
Bw. Mchechu alisema pamoja na Ofisi kuongeza mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 30 hadi kufikia Sh1.327 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa kuweka malengo yanayochochea ubunifu na utendaji wa hali ya juu.
Alieleza kuwa taasisi itaendelea kuweka malengo yenye mwelekeo wa kuongeza thamani kwa Serikali huku ikizingatia uhalisia wa mazingira ya utekelezaji.
Aidha, alisema kuimarika kwa utendaji na hali ya kifedha ya taasisi na kampuni ambazo Serikali ina uwekezaji, kumeongeza uwezo wa Serikali kupata gawio na faida kubwa zaidi.
Aliongeza kuwa OTR inaendelea kuimarisha mifumo ya tathmini ya utendaji kwa kushirikiana na wataalamu wa nje ili kujifunza mbinu bora za kimataifa zitakazosaidia kuboresha usimamizi wa taasisi za umma na kuongeza ufanisi wake kwa muda mrefu.
Kwa upande mwingine, Bw. Mchechu alisema Ofisi inaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ubora ikiwemo utekelezaji wa viwango vya ubora (ISO) na kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu.
Alisema hatua hizo zitawezesha kuwepo kwa taratibu zinazofanana katika utoaji wa huduma, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha taasisi za umma zinaendelea kujiendesha kwa ufanisi, tija na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.