Waziri Mkumbo atembelea mashamba manne ya Serikali
Na Mwandishi wa OTR
Kilimanjaro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, leo ametembelea mashamba manne yanayomilikiwa na Serikali na kusimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Lengo la ziara hiyo ni kuangalia tija ya matumizi ya mashamba hayo kwa manufaa ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi, Kijiji cha Endumeki, Prof. Mkumbo alisema uwekezaji si lazima utokane na wawekezaji wa nje ya nchi, akisisitiza kuwa Serikali itahakikisha rasilimali zake zinaendelezwa na kutumika kwa tija kwa manufaa ya Taifa na wananchi.
Aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Siha kuwa, pamoja na Serikali kuendelea kuvutia wawekezaji, itaendelea kulinda masilahi ya wananchi wa Siha.
Ofisi ya Msajili wa Hazina, inasimamia kwa niaba ya Serikali, jumla ya mashamba 10, ambayo ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kilimo cha kibiashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Mashamba hayo yamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza linahusisha mashamba sita yaliyokuwa yanamilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Kilimo (NAFCO) na yaliyosalia wakati wa zoezi la ubinafsishaji kufuatia maelekezo ya Mhe. Rais ya kusitisha uuzaji wake ili Serikali iyaendeleze kwa tija.
Mashamba hayo ni Basotu, Hanang, Namtumbo, Ruvuma Harlington, Journey’s End Fosters na Kanamodo, yote yaliyopo West Kilimanjaro.
Kundi la pili linahusisha mashamba manne yaliyonunuliwa na Serikali kupitia taratibu mbalimbali kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Mashamba hayo ni KPL Mng’eta lililopo Morogoro, Shamba la Maua la Malalua lililopo Arusha, Kiliflora Usa River na Kiliflora Chekereni, yote yaliyopo Arusha.