Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Serikali yaokoa Sh13 bilioni kutokana na matumizi ya NeST
12 May, 2025
Serikali yaokoa Sh13 bilioni kutokana na matumizi ya NeST

 

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Serikali imeokoa Sh 13.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24, kutokana na matumizi ya mfumo wa ununuzi wa umma kidijitali (NeST), mfumo uliobadili matumizi ya karatasi katika maandalizi na ukamilishaji wa zabuni.

 

Bw. Dennis Simba, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) alisema Mei 12, 2025 kuwa kiasi hicho kilichookolewa ni gharama ambazo zingetumika katika ununuzi wa karatasi kwa ajili ya maandalizi na ukamilishaji wa zabuni.

 

Bw. Simba, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

 

Kwa mujibu wa utafiti wa awali uliofanywa na PPRA, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 pekee, matumizi ya mfumo wa NeST umesaidia kupunguza metriki tani 617.85 za utoaji wa kaboni angani kutokana na kuachana na matumizi ya karatasi.

 

Bw. Simba alisema matumizi ya mfumo huo ulioanza kutumika nchi nzima Julai 1, 2023 na kuzinduliwa rasmi Septemba 9, 2024 na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dk. Doto Biteko, umeongeza ufanisi wa taasisi za umma.

 

“Mfumo umepunguza muda wa taasisi nunuzi kupitia taarifa za mzabuni hivyo kupunguza muda wa uchakataji wa zabuni,” alisema.

 

 

Aliongeza: "Kupunguza muda wa uchakataji wa zabuni na uwepo wa nyaraka za zabuni ndani ya mfumo kumepunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao taasisi nunuzi walikuwa wanatumia wakati wa uandaaji wa zabauni.”

 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri aliwataka waandishi wa habari kutumika kama daraja la kuwafikishia wananchi mambo mazuri  yanayofanywa na serikali.

 

“Waandishi wa habari ni kiungo muhimu sana cha serikali na wananchi. Naomba mkatumie vema kalamu zenu ili wananchi walishwe kile wanachostahili,” alisema Bw. Sabato.