Msajili wa Hazina apongeza taasisi ya Mandela kwa tafiti nzuri na ubunifu

Arusha. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu ameimwagia sifa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kufanya vizuri katika eneo la ubunifu na tafiti mbalimbali zinazotoa matokeo chanya kwa jamii.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kujionea jinsi inavyotekeleza majukumu yake, Jumatatu (Oktoba 21, 2024) Tengeru, jijini Arusha, Bw. Mchechu alisema Taasisi hiyo inapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee.
“Inabidi tuiangalie taasisi hiyo kwa jicho la tofauti kwasababu ni taasisi pekee iliyojikita katika kufanya tafiti na kutoa taaluma kwa ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu,” alisema Bw. Mchechu.
Aliongeza: “Taasisi hii ni muhimu kwetu, kwasababu ili maendeleo yaweze kupatikana lazima sayansi na Teknolojia ihusike.”
Alisema ni wakati muafaka kwa nchi kupitia taasisi zake ikiwemo Nelson mandela, kuwa wabunifu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Bw. Mchechu aliahidi kushrikiana kwa karibu na taasisi hiyo ya Sayansi na Teknolojia ili tafiti na bunifu zinazozalishwa ziwafikie walengwa na kukidhi soko la ndani na nje.
Alieleza haja ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanzisha kitengo kitakachounganisha watafiti, uhamasishaji rasimali na ubiasharishaji, ili kuwezesha tafiti zinazofanyika kuwafikia walengwa na hatimaye kukuza uchumi wa Taasisi na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Maulilio Kipanyula, alisema taasisi ya Nelson Mandela ni kiota cha sayansi , teknolojia na ubunifu katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani na nje ya nchi kupitia bunifu zake.
“Tumefarijika na ujio wa Msajili wa Hazina kwani ziara yake ni muendelezo katika kuleta mageuzi ya kiutendaji katika taasisi za umma,” alisema Bw. Mchechu.
Akiwa ziarani, Msajili wa Hazina alipata wasaa wa kutembelea maeneo mbalimbali ya kiutendaji wa Taasisi hiyo ikiwemo Kituo cha Elimu Kidigitali (C-CoDE), Maktaba, Maabara, Kituo cha TEHAMA (HPC), kituo Atamizi (Incubation Centre), Kiwanda kidogo (DDI) pamoja na mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi.
Habari hii imeandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina.