Wakurugenzi Ofisi ya Msajili wa Hazina wapigwa msasa kwa siku tano
Na Mwandishi wa OMH
Kibaha. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IoDT) imeendesha mafunzo maalum ya uongozi na usimamizi kwa Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi hiyo, yakilenga kuimarisha uwezo wa menejimenti katika kusimamia rasilimali za umma kwa weledi, uwajibikaji na kwa maslahi mapana ya taifa.
Mafunzo hayo ya siku tano yamefanyika kuanzia Februari 2 hadi 6, 2026 katika Shule ya Uongozi ya Mwl. Julius Nyerere iliyopo Kibaha, yakiwa na dhima kuu ya “Uongozi na Usimamizi Wenye Uwajibikaji kwa Maslahi ya Taifa”.
Kupitia programu hiyo ya siku tano, washiriki walipata fursa ya kujifunza na kujadiliana masuala ya msingi ya uongozi wa kimkakati, utawala bora, uzalendo, maadili ya uongozi wa umma, pamoja na ulinzi wa taasisi dhidi ya hatari za kiutendaji, kimaadili na kiusalama.
Miongoni mwa mada zilizofundishwa ni pamoja na misingi ya utawala bora, uongozi unaozingatia uwajibikaji na matokeo, usimamizi wa uwekezaji wa umma, maamuzi ya kimkakati katika kusimamia taasisi na mashirika ya umma, pamoja na uongozi unaojengwa juu ya maslahi ya taifa na usalama wa nchi.
Aidha, washiriki walijengewa uwezo katika maeneo ya itifaki na adabu kwa viongozi, usimamizi wa hisia (emotional intelligence), majadiliano ya kimkakati, pamoja na uwasilishaji na taswira ya kiongozi katika ngazi ya juu ya Serikali.
Mafunzo hayo pia yaliangazia masuala yanayoathiri uongozi wa kisasa, ikiwemo matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali serikalini, uelewa wa bodi mtandao (e-Board), pamoja na misingi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) kwa viongozi, hususan fursa, changamoto na masuala ya kimaadili katika maamuzi ya kimkakati.
Vilevile, mada za afya ya viongozi, usimamizi wa msongo wa mawazo na uimara wa kiongozi zilijadiliwa kwa lengo la kuhakikisha ufanisi endelevu wa viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wa manufaa, mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza mshikamano na ulinganifu wa uongozi ndani ya OMH, kuboresha ubora wa maamuzi ya menejimenti, na kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa hisa na mali za umma zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kupitia uelewa wa pamoja wa dhima ya uongozi na ulezi wa taasisi (institutional stewardship), Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wamejengewa msingi imara wa kusimamia taasisi na mashirika ya umma kwa ufanisi, nidhamu na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Kwa ujumla, ushirikiano kati ya OMH na IoDT katika mafunzo haya ni hatua muhimu katika kujenga uongozi thabiti wa kimkakati ndani ya Serikali, unaoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya usimamizi wa rasilimali za umma, na unaochangia moja kwa moja katika kuimarisha utendaji wa OMH kama msimamizi mkuu wa maslahi ya Serikali katika taasisi na mashirika ya umma.