Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Msajili wa Hazina aikaribisha Jeune Afrique Media Group kuangazia fursa za uwekezaji Tanzania
09 Feb, 2026
Msajili wa Hazina aikaribisha Jeune Afrique Media Group kuangazia fursa za uwekezaji Tanzania

Na Mwandishi wa OMH

 

Leo, Februari 9, 2026, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Frederic Van de Vyver, Mkuu wa Anglophone Africa Jeune Afrique Media Group, kampuni inayoongoza ya habari ya Kipanafrika yenye makao makuu jijini Paris, Ufaransa.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, walijadiliana namna wanavyoweza kushirikiana katika fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.

 

Bw. Mchechu alimhakikishia Bw. Van de Vyver kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba atapata ushirikiano wa kutosha.

 

“Kwa upande wa sekta ya umma, utapata ushirikiano wa kutosha kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, na kwa upande wa sekta binafsi utapata ushirikiano kupitia CEO Roundtable ya Tanzania (CEOrt),” alisema Bw. Mchechu.

 

Kwa upande wake, Bw. Van de Vyver alieleza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania.

 

“Ni lazima tutafute njia bora za kushirikiana,” alisema, huku akikubaliana na Msajili wa Hazina kwamba Tanzania ina mazingira rafiki kwa biashara.