Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Jinsi ya kuongeza mchango wa mapato yasiyo ya kodi
22 Oct, 2024
Jinsi ya kuongeza mchango wa mapato yasiyo ya kodi

 

Dar es Salaam. Mwezi Agosti mwaka huu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alieleza shauku yake ya kutaka kuona mapato yasiyo ya kodi kutoka kwa Mashirika ya Umma na yale ambayo serikali ina hisa chache yanachangia asilimia kumi ya mapato ya ndani katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

 

Kwa sasa, mchango wa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) uko katika asilimia tatu, na ni katika muktadha huu, wachambuzi wanatoa maoni yao ya namna ya kuongeza mchango wa mashirika hayo.

 

 

Wachumi walioongea na Ofisi ya Msajili wa Hazina hivi karibuni wana mtazamo kwamba hakuna miujiza itakayofanyika ili kuongeza mapato yasiyo ya kodi, isipokuwa kwa kuongeza wigo wa vyanzo vya mapato yasiyo ya kodi.

 

Ikichangia wastani wa asilimia 47 katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, gawio ndio chanzo kikubwa cha mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

 

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Abel Kinyondo, alisema ili serikali ipate mapato zaidi, kupanua vyanzo vya mapato ni lazima.

 

“Tunaweza kupanua wigo wa mapato yasiyo ya kodi kwa kupanua sekta ya uchumi rasmi,” alisisitiza Prof. Kinyondo.

 

Aliendelea kuongeza: “Uchumi wetu rasmi ni mdogo sana. Serikali inapaswa kuendelea kutengeneza  mazingira mazuri ya biashara ambayo yatatoa sababu kwa walio nje ya sekta isiyo rasmi kujiunga na sekta rasmi.”

 

Hiki ndicho serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikifanya tangu mkuu huyo wa nchi aliposhika hatamu tarehe 31 Machi 2021.

Katika hili, ni dhahiri shahiri, Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa, na takwimu zinaongea zenyewe, na siku zote huwa haziongopi.

 

Mbinu ya serikali ya kuwa bega kwa bega na wafanyabiashara inapeleka ujumbe mzuri kwa wawekezaji, huku takwimu za hivi karibuni zikionesha ongezeko la asilimia 53 katika thamani ya miradi iliyosajiliwa mwaka jana.

 

Kulingana na Ripoti ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 2023 iliyozinduliwa katikati ya Septemba mwaka huu, idadi ya miradi iliyosajiliwa mwaka jana ilikuwa na thamani ya $8,658 milioni ikilinganishwa na $5,658.47 milion zilizowekezwa mwaka 2022.

 

Idadi ya miradi iliyosajiliwa kutoka sekta mbalimbali mwaka jana iliongezeka kwa asilimia 15.2 hadi kufikia 9,678.

 

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. Daudi Ndaki, alishauri kwamba serikali inapaswa kuendelea na juhudi za kuboresha mazingira ya biashara, ili kuvutia zaidi wawekezaji katika sekta rasmi.

 

Alieleza kwamba serikali inapaswa kutumia wataalamu kupanga mikakati ya jinsi ya kukusanya vyanzo vilivyopo vya mapato kwa ufanisi, lakini bila kumuumiza mtu yeyote.

 

Zaidi ya hayo, Dkt. Ndaki aliongeza, wataalamu hao hao wanapaswa kusaidia serikali katika kubuni vyanzo vipya vya mapato yasiyo ya kodi ili iweze kupata zaidi bila kubebesha mzigo wachache.

 

Huu pia umekuwa ni wimbo wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.

 

Mkuu huyo wa nchi amenukuliwa mara kadhaa akisema: “Tunahitaji mfumo rafiki wa kodi ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje. Tunahitaji biashara zistawi na watu wafurahie matunda.”

 

Tukirudi kwa Dkt. Ndaki, pia alishauri kwamba, sehemu kubwa ya fedha za mashirika ya umma inapaswa kuelekezwa katika shughuli za msingi za mashirika hayo ili kuwa na ufanisi na kuzalisha mapato zaidi.

 

 Msajili wa Hazina, Bwana Nehemiah Mchechu, amenukuliwa mara kadhaa akitoa ahadi ya kufanya lolote liwezekanalo kuboresha utendaji wa mashirika ya umma ili yaongeze ukusanyaji wa mapato na hatimaye mchango wao katika mfuko mkuu wa serikali.

 

“Tumejizatiti kuongeza ufanisi wa mashirika ya umma kwa kuboresha usimamizi wa mashirika hayo,” alisema Bwana Mchechu.

 

Aliongeza: “Hii itakuwa kichocheo cha kuyapeleka mashirika ya umma kwenye kiwango cha juu zaidi,” Bwana Mchechu alionyesha matumaini yake.

 

Hivi karibuni Bw. Mchechu alisema ofisi yake inahitaji zaidi mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na shughuli za uzalishaji kuliko faini na adhabu.

 

“Tunahitaji kuhakikisha mchango mzuri na endelevu wa mashirika ya umma katika maendeleo ya kitaifa kwa kuzingatia ubora wa uendeshaji na uwezo wa kibiashara,” alisisitiza.

 

Aliendelea kusema: “Faini na adhabu hazina afya kwa uchumi wetu. Tunahitaji kuja na mikakati itakayopanua vyanzo vyetu vya mapato yasiyo ya kodi.”

 

Dkt. Tobias Swai, Mkuu wa Idara ya Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliiambia ofisi ya Msajili wa Hazina kwamba ikiwa itataka kuongeza mapato yasiyo ya kodi, mashirika ya umma yanapaswa kuwekeza katika biashara zinazotumiwa na sehemu kubwa ya Watanzania.

 

Akitaja baadhi ya maeneo ambayo mashirika ya umma yanapaswa kuwekeza kwa nguvu, kama sekta ya fedha na bima, utalii, usafirishaji wa abiria na mizigo, pamoja na kilimo, alionya kwamba uwekezaji unapaswa kwenda sanjari na ufanisi katika utoaji wa huduma.

 

“Ni wakati muafaka kwa serikali kuboresha mashirika ya umma ili yaweze kuwa katika nafasi ya kutumia vilivyo fursa zilizopo,” alisisitiza Dkt. Swai.

 

Aliendelea kuongeza: “Tunahitaji mifumo ya uongozi thabiti. Tunahitaji uwazi katika ajira za mashirika yanayojiendesha kibiashara.”

 

Makala hii imeandaliwa na

Ofisi ya Msajili wa Hazina.