Watanzania waonesha uwezo katika kampuni za ubia
Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Tanzania inashuhudia mabadiliko makubwa na ya kimkakati katika uongozi wa kampuni za ubia, ambapo watanzania sasa wanashika nafasi za juu za uongozi katika taasisi muhimu ambazo awali ziliongozwa na wataalamu kutoka nje ya nchi.
Kwa miaka mingi, kampuni nyingi zenye hisa za serikali pamoja na wawekezaji wa kimataifa zilitegemea viongozi wa kigeni katika nafasi za juu za usimamizi, yaani Afisa Mtendaji Mkuu.
Lakini sasa upepo umegeuka — Watanzania wanapewa nafasi, na matokeo yake yanaonekana wazi, kifedha na kimkakati.
Mabadiliko haya yanaonekana katika taasisi kama Benki ya NMB, Benki ya NBC, Kampuni ya Mafuta ya Puma (Puma Energy Tanzania) na Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER).
Kampuni hizi, ambazo awali ziliongozwa na wageni, sasa zinaongozwa na Maafisa Watendaji Wakuu wazawa wenye weledi mkubwa na uelewa wa kina kuhusu mazingira ya kiuchumi ya Tanzania.
Hatua hii inaendana na dira ya serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) chini ya Bw. Nehemiah Mchechu.
Lengo ni kuhakikisha Watanzania wanapewa nafasi si kwa jina tu, bali kwa matokeo yenye tija, uwajibikaji na faida kwa taifa.
“Lengo letu si kuweka wazawa tu katika nafasi za juu, bali kuhakikisha uongozi huo unaleta matokeo, uwajibikaji na manufaa ya muda mrefu kwa taifa,” alisema Bw. Mchechu.
Matokeo halisi ya uongozi wa wazawa
Katika Benki ya NBC, uongozi wa Bw. Theobald Sabi, aliyeteuliwa mwaka 2018 kuchukua nafasi ya Mwingereza Edward Marks, umeleta mageuzi makubwa.
Chini ya uongozi wake, gawio la serikali limeongezeka kutoka Sh1.3 bilioni hadi Sh10.5 bilioni, ongezeko la asilimia 707.7.
Katika Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna — Mtanzania wa kwanza kushika nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu — ameongoza mabadiliko makubwa tangu alipoteuliwa mwaka 2020.
Chini ya uongozi wake, gawio la serikali limeongezeka kutoka Sh16 bilioni hadi Sh68.1 bilioni, ongezeko la asilimia 325.6.
Amejikita katika mageuzi ya kidijitali, upanuzi wa huduma za kifedha jumuishi na ukuaji endelevu — mambo yaliyoiweka NMB katika nafasi ya juu kibiashara.
Katika sekta ya nishati, Bi. Fatma Abdallah aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania mwezi Januari 2023, akichukua nafasi ya raia wa Afrika Kusini, Dominic Dhanah.
Akiwa na uzoefu wa kimataifa kutoka ofisi za Puma jijini Geneva, ameongeza gawio la serikali kutoka Sh8 bilioni hadi Sh13.5 bilioni, ongezeko la asilimia 68.8.
Kwa upande wa TIPER, kampuni ya ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Oryx Energies SA, Januari 2023 ilimteua kwa nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. Mohamed Mohamed, kuchukua nafasi ya Mfaransa Daniel Belair.
Chini ya uongozi wake, gawio la serikali limepanda kutoka Sh1.5 bilioni hadi Sh5.5 bilioni, ongezeko la asilimia 267, na kuifanya TIPER kuwa nguzo muhimu katika sekta ya uhifadhi mafuta nchini.
Uthibitisho wa mafanikio
Kufikia Juni 9, 2025, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa imekusanya Sh1.028 trilioni kutoka kwenye gawio na michango ya taasisi za umma na kampuni za ubia — ongezeko la asilimia 68 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, na asilimia 34 zaidi ya makusanyo ya jumla ya mwaka wa fedha 2023/24.
Kwa mujibu wa Bw. Mchechu, matokeo haya si bahati nasibu, bali ni zao la sera makini inayochochea uongozi wa kizalendo katika kampuni ya ubia.
“Tunaona enzi mpya ya imani kati ya serikali na washirika wake. Wawekezaji wa kimataifa wana imani na viongozi wa Kitanzania — na matokeo yanaonyesha ukweli huo,” alisema.
Sera mpya ya ubia wa ushindi kwa pande zote
Akizungumza katika siku ya gawio iliyofanyika Juni 10, 2025, Mhe. Rais Dk. Samia alisisitiza dhamira ya serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika maeneo yenye umuhimu wa kimkakati.
“Ubia wetu lazima ufuate mfumo wa ‘win-win’ — kuhakikisha serikali na wawekezaji wote wanapata manufaa,” alisema Mhe. Rais.
Kauli hiyo inaimarisha msimamo wa serikali kupitia OMH katika kusimamia uwekezaji wa umma kwa weledi na uwazi, huku ikihakikisha Watanzania wenye uwezo wanapewa nafasi za uongozi katika kampuni yenye ushiriki wa serikali.