Uvutiaji na ukumbatiaji talanta: Muhimu kwa ufanisi wa taasisi za umma
Dar es Salaam. Kadri mazingira ya kazi duniani yanavyobadilika, mafanikio ya taasisi za umma yanaendelea kutegemea zaidi kipengele kimoja muhimu: talanta.
Usimamizi wa rasilimali watu kwa ubunifu, mtazamo wa kimkakati, na ustahamilivu umehama kutoka kuwa jambo la hiari, kuwa muhimu kwa uendelevu wa muda mrefu wa taasisi za umma.
Bila ya kuwa na watu sahihi, sera, mipango, na huduma zinazolenga kuboresha jamii ziko hatarini kutokufanikiwa au kudumaa.
Katika muktadha huu, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikisisitiza mara kwa mara juu ya umuhimu wa Taasisi za Umma kuvutia, kukumbatia, na kukuza talanta za kiwango cha juu.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, hivi karibuni alisisitiza umuhimu wa kuwa na wafanyakazi wenye ujuzi, hasa katika sekta ya umma ambapo rasilimali mara nyingi ni chache.
“Wafanyakazi wanaohisi kuhusishwa na lengo kubwa la taasisi huwa na uwezekano mkubwa wa kufanya kazi kwa moyo wote, hasa wanapoona michango yao inakuwa na athari chanya katika jamii zao,” alibainisha.
Bw. Mchechu alitaja baadhi ya mambo muhimu yanayo changia wafanyakazi kufungamana na taasisi zao kwa moyo wote: maendeleo ya kitaaluma, usawa kati ya kazi na maisha binafsi, na uongozi imara.
Vipengele hivi hutengeneza mazingira ya wafanyakazi kuona wanathaminiwa na kuwa na motisha ya kusalia katika taasisi na kufanya kazi kwa bidii kulingana na dhamira na maono ya taasisi husika.
Pia alitoa tahadhari kwamba bila ya talanta sahihi, hata mipango yenye nia nzuri haiwezi kuleta tija kwa taasisi za umma.
“Talanta ina umuhimu mkubwa sana, ikiwa tunataka kuzipeleka taasisi za umma kwenye kiwango kingine bora zaidi,” alisema Bw. Mchechu, akisisitiza kuwa uvutiaji na uhifadhi wa talanta haupaswi kutazamwa kama jitihada za muda mfupi, bali kama uwekezaji wa muda mrefu.
Taasisi za umma lazima zitengeneze mazingira ya mafunzo ambayo yatawawezesha wafanyakazi kuendana na mazingira yanayobadilika kila wakati.
Dkt. Lufunyo Hussein, Mkuu wa Chuo cha Bandari cha Dar es Salaam, hivi karibuni alisisitiza haja ya taasisi za umma kutambua kuwa usimamizi bora wa talanta haumaliziki kwa kujaza nafasi za kazi tu.
Alisema taasisi za umma zinapaswa kuzingatia kukuza utamaduni unaowapa wafanyakazi uwezo wa kubuni, kukua, na kubaki na shauku ya kufanya kazi katika taasisi husika.
Dkt. Hussein pia alishauri kwamba Wakuu wa Taasisi za Umma waone wafanyakazi siyo tu kama ni uwekezaji mkubwa wa shirika, bali kama kichochea kikuu cha mafanikio ya kimkakati.
“Viongozi wa taasisi za umma lazima waweke talanta katika kiini cha mkakati wa biashara zao, ikiwa wanataka kupata matunda ya uwekezaji,” aliongeza.
Alisisitiza: “Tunahitaji kukuza talanta na siyo kuua talanta.”
Kwa mujibu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), mikakati bora ni muhimu sio tu kwa kuwabakisha wafanyakazi waliopo, bali pia kwa kuvutia talanta mpya.
Ripoti ya OECD inasema: "Uzoefu wa kwanza wa watu kuhusu mahali una nafasi kubwa katika kuamua ikiwa wataendelea kubaki au la na ikiwa watakuwa tayari kueneza habari njema kwa wengine."
Mtazamo huu unaonesha kuwa taasisi za umma lazima ziwekeze katika kuunda utamaduni chanya na wa kiujumuishi kazini, utamaduni utakaowavutia wafanyakazi na wale wanaotarajia kujiunga na taasisi husika siku za mbeleni.
Kama vile mwandishi wa vitabu maarufu, Peter Drucker, alivyosema: "Njia bora ya kutabiri siku zijazo ni kuziumba."
Falsafa hii inasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ukuaji wa wafanyakazi leo ili kuunda shirika imara huko mbeleni.
Makala hii imeandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina