Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Puma Energy yazindua kituo kikubwa zaidi cha CNG barani Afrika
12 Feb, 2026
Puma Energy yazindua kituo kikubwa zaidi cha CNG barani Afrika

 

Na Mwandishi wa OMH

Dar es Salaam: Mapema wiki hii, kampuni ya Puma Energy Tanzania, ambayo Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inamiliki asilimia 50 ya hisa ilizindua rasmi Kituo Mama cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) ambacho ni kikubwa na cha kisasa zaidi barani Afrika.

 

Kituo hicho cha kihistoria kilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, tukio linaloashiria hatua kubwa katika safari ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati safi, nafuu na ya uhakika.

 

Kikiwa jijini Dar es Salaam, kituo hiki cha kisasa kimeundwa kukidhi ongezeko la mahitaji ya CNG, ambayo ni mbadala nafuu na rafiki kwa mazingira badala ya mafuta ya petroli na dizeli.

 

Kituo hicho kitahudumia magari madogo, mabasi, na malori makubwa, huku kikifanya kazi kama kitovu cha usambazaji wa gesi kwenda vituo vingine vidogo vya CNG nchini kupitia trela maalum za kusafirisha gesi (tube-trailers).

 

Kituo hiki Mama cha CNG ni zaidi ya miundombinu; ni ishara ya imani yetu ya muda mrefu kwa Tanzania na dhamira yetu ya kuleta thamani kwa pamoja. Tunajivunia kushirikiana na Serikali kutekeleza mradi utakaoliendesha taifa mbele kwa miaka mingi ijayo,” alisema Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania.

 

Kituo hiki kipya kina uwezo wa kuhudumia aina mbalimbali za vyombo vya usafiri, ikiwemo magari madogo, mabasi na malori makubwa.

 

Aidha, kitafanya kazi kama kitovu kikuu cha kusambaza CNG kwa vituo vingine vidogo nchini kupitia trela maalum za gesi.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameusifu mradi huo kuwa mfano thabiti wa mafanikio ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji na kutumia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) kwa maendeleo ya Taifa.

 

Puma Energy Tanzania ni mfano mzuri wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ikitoa huduma bora za nishati huku ikichangia mapato ya Serikali, ajira, na ujenzi wa miundombinu ya kimkakati.

 

Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji huu unaendana kikamilifu na vipaumbele vyetu vya kitaifa,” alisema Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Akiongea kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, Bw. Linus Kakwesi aliunga mkono kauli hizo akibainisha kuwa muundo wa kipekee wa umiliki wa kampuni hiyo unahakikisha mafanikio ya kibiashara yanatafsiriwa moja kwa moja kuwa manufaa ya Taifa.

 

Ubia huu unaonesha kuwa kuunganisha ushiriki wa Serikali na ufanisi wa sekta binafsi kunaleta miundombinu muhimu na faida kubwa za kifedha kwa Watanzania,” alisema Bw. Kakwesi ambaye ni msaidizi wa Msajili wa Hazina.

 

Katika kipindi cha ujenzi wa mradi huu, zaidi ya ajira 300 zilitolewa kwa Watanzania pekee, ikiwemo nafasi 100 za kitaalamu kwa wahandisi na mafundi.

 

Mradi pia uliwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani na biashara ndogo na za kati (SMEs), na hivyo kuingiza mtaji mkubwa katika uchumi wa eneo husika.

 

Kituo hiki kinapoanza kufanya kazi kikamilifu, kitaendelea kutoa ajira za kudumu na kuwezesha uhamishaji muhimu wa ujuzi katika sekta ya gesi asilia inayokua kwa kasi.

 

Uwekezaji huu ni sehemu ya dhamira ya muda mrefu ya Puma Energy nchini Tanzania.” alisema Wakili Emmanuel Bakilana, Mkuu wa Idara ya Sheria na Mahusiano ya Puma Energy Tanzania. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kampuni imelipa zaidi ya Sh1.4 kama kodi na ushuru mbalimbali.

 

Mwaka 2025, kampuni ilitangaza gawio la Sh21 bilioni kwa wanahisa.