Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Rais Samia Apigilia Msumari Uanzishwaji Mfuko wa Uwekezeji wa Umma
04 Sep, 2024
Rais Samia Apigilia Msumari Uanzishwaji Mfuko wa Uwekezeji wa Umma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma huku akiwataka wanaosimamia sheria ya uanzishwaji wake kuwaelimisha wananchi na ikiwezekana Mfuko huo uundiwe sheria ya peke yake.

 

Mhe. Rais Samia ametoa msisitizo huo jana Agosti 28, 2024 jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha pili cha mwaka cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.

 

Alisema kuwa, kuna baadhi ya watu wanaona kama unaanzishwa mfuko wa pili wa hazina lakini sio kweli kwani nchi nyingi duniani kuna mifuko ya aina hiyo ambayo inazisaidia taasisi na mashirika ya umma kusonga mbele.

 

"Fedha zitakazowekwa kwenye Mfuko huo sio kwa ajili ya tuliopo leo bali ni kwa ajili ya vizazi vinavyokuja, tunawajengea msingi. Hata kama itatumika sasa lakini itatumika tukijua ya kwamba ni uwekezaji ambao utaleta faida na kukuza mfuko kwa ajili ya hazina ya baadaye", alisema Rais Samia.

 

Amefafanua kuwa, Mfuko huo utasaidia kupunguza kutegemea wawekezaji kutoka nje na utasaidia nchi kuanza kujenga utajiri wake hivyo amewataka wanaosimamia Mfuko huo kuwaita watu kutoka kwenye nchi ambazo zimefanya vizuri na kuelekeza  jinsi walivyotekeleza hilo.

 

"Taasisi na Mashirika ya umma, huu ndio Mfuko ambao mtatakiwa kuuchangia sana kwa sababu fedha itawekezwa na kuleta faida." Alimalizia Rais Samia.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari hivi karibuni, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alisema kuwa Mhe. Rais aliagiza kufanyika mabadiliko ya kisheria ambayo yatasaidia kuimarisha uendeshaji wa taasisi na mashirika ya umma.

 

"Moja ya mabadiliko ya sheria yanayofanyiwa kazi ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma utakaokuwa unatunza mitaji kwa ajili ya kuzisaidia taasisi na mashirika ya umma pale yanapokuwa yanahitaji kuwekeza na hayana fedha." Alisema Mchechu.