OMH inakusudia kufanya kazi kama kampuni mama 'Holding company'

Dar es Salaam. Ni nini kingetokea kama Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) ingekuwa inafanya kazi kwa kutumia zaidi mfumo wa kampuni mama yaani ‘holding company’?
Hili ndio swali linalochagiza mabadiliko makubwa yanayoendelea katika Ofisi hiyo linapokuja suala la utendaji na usimamizi wa mashirika ya Umma.
Ikiwa na lengo la kupata matokeo chanya kutokana na uwekezaji wa Sh86.3 trilioni katika Mashirika ya Umma na Kisheria, pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache, OMH imejizatiti kufanya mageuzi makubwa katika ufanyaji kazi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa taasisi za umma.
Uwekezaji huo ambao serikali inataka kuona wananchi wananufaika nao, umefanywa katika Mashirika ya Umma na Kisheria 253, pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache 56.
Nyuma ya mabadiliko makubwa ya namna Ofisi ya Msajili wa Hazina inataka kufanya kazi na taasisi za umma, ni Bw. Nehemiah Mchechu, ambaye ni Msajili wa Hazina.
Kufanya kazi kwa mfumo wa kampuni mama, kutaifanya OMH kujikita zaidi kwenye usimamizi wa mashirika ya umma, badala ya kujihusisha moja kwa moja katika utendaji kazi wao kama mdhibiti, mara kadhaa Bw. Mchechu amenukuliwa akisema.
Ili kuunga mkono mabadiliko haya, serikali, kupitia OMH, inatambua umuhimu wa kuyapa uhuru zaidi mashirika ya kimkakati na yale yenye mlengo wa kibiashara.
Kwa kuruhusu mashirika haya kufanya kazi kwa uhuru zaidi katika maeneo fulani, OMH inakusudia kuimarisha uwezo wao wa kufikia malengo yao kwa ufanisi kwani wanakuwa kwenye nafasi ya kuwa wabunifu zaidi.
“Tunataka kuyapatia uhuru zaidi mashirika ya umma ili kutoa nafasi ya kufanya ubunifu zaidi na hivyo kuleta tija kwa nchi yetu,” Bw. Mchechu alisema hivi karibuni.
Ili kuhakikisha kwamba uhuru huu unaleta matokeo chanya, OMH itazingatia vigezo vya kutambua mashirika yanayostahili kupewa uhuru na kupima matokeo ya uhuru huu.
Mzizi wa Serikali, kupitia OMH, kufikiria mpango huu wa kufanya kazi kama kampuni mama, ni kutofanya vizuri kwa mashirika ya umma na hivyo kuwa na mchango mdogo kwenye uchumi wa nchi.
Kwa sasa mchango wa mapato yasiyo ya kikodi yanayo kusanywa na OMH kutoka kwa Mashirika ya Umma na Kisheria, pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache, ni asilimia tatu tuu ya mapato ya ndani.
Kutokana na mchango kuwa mdogo, mwezi Agosti Mwaka jana, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maelekezo kutaka mchango wao uongezeke hadi kufikia asilimia 10 ndani ya miaka mitano.
Ili kufikia azma hiyo, Bw. Mchechu alisema: “Tumedhamiria kutengeneza mazingira rafiki kwa mashirika haya ya umma ili yaweze kustawi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa letu.”
Mara kwa mara Bw. Mchechu amekuwa akisisitiza kwamba katika uongozi wake, OMH haitajiangalia kama mdhibiti, bali kama mbia wa taasisi za umma.
Tafsiri ya hii ni kwamba ana maono ya kuwa na ofisi ambayo itajiona kuwa sehemu ya taasisi za umma na hivyo kutengeneza mazingira wezeshi yatakayo ongeza ufanisi.
“Ofisi yangu inapaswa kufanya kazi kama kampuni mama,” alisisitiza hivi karibuni, akionesha haja ya ushirikiano, huku heshima ya mamlaka ya OMH ikibaki palepale.