Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Mchechu tumia ‘rungu’ la Samia kuboresha Mashirika ya Umma
28 Jun, 2024
Mchechu tumia ‘rungu’ la Samia kuboresha Mashirika ya Umma

Na Mwandishi Dar es Salaam,

 

“KWENYE mageuzi haya Mchechu na Waziri wako lazima muwe unpopular, sijawahi kusikia Waziri wa Fedha akasifiwa hata siku moja, siku zote Waziri wa Fedha analaaniwa, kwahiyo Mchechu na wewe utalaaniwa tu hapa, na nyingine zitakuja personal, nyingine kikazi, lakini hii ndiyo kazi niliyokupa, simama na ifanye.”

 

Hii ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, aliyoitoa jijini Dar es Salaam Juni 11, 2024 wakati akipokea Gawio la Serikali kutoka kwa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo Serikali ina hisa kidogo.

 

Rais Samia, ambaye ni muumini wa mageuzi ya kiuchumi, alitoa kauli hiyo wakati akirejelea takwimu zilizotolewa siku hiyo wakati anapokea gawio la jumla ya Shs. 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio la Shs. 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango Shs. 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine, yakiwa ni makusanyo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi mwezi

Mei 2024.

 

Na ndiyo maana akasema, yeye binafsi anatukanwa sana mitandaoni, lakini amejigeuza chura anajifanya hasikii na wala hatojibu bali anachotaka yeye ni mageuzi ya kiuchumi ili kuipeleka Tanzania mbele.

 

Lakini Rais Samia akatoa mifano ya jitihada zake namna zinavyozaa matunda, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo wengi walimbeza na kuzua taharuki alipokaribisha uwekezaji wa kampuni ya DP World kutoka Dubai, ikiwa kinara katika ongezeko la gawio mwaka huu.

 

Akasema: "Wale waliopiga kelele Mama kauza bahari, Mama kauza bandari, Mama kauza nini - mauzo yale faida yake ni hii leo (TPA kuongeza mapato). Huu ni mwanzo, tunatarajia mtapata faida kubwa zaidi kwa bandari zetu kubwa zote ambazo ziko nchini."

 

TPA iliongoza kundi la taasisi zisizo za biashara lilonajumuisha Mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mashirika ya Umma zinawajibika kutoa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi baada ya kutoa gawio la Shs. bilioni 153.9, ikifuatiwa kwa mbali sana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa Shs. bilioni 34.7, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) iliyotoa Shs. bilioni 21.3, Wakala wa Huduma za Meli (TASAC) ilitoa Shs. bilioni 19.1, na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ukatoa Shs. bilioni 18.9.

 

Kwa kundi la taasisi za kibiashara linalojumuisha Mashirika na Kampuni ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Makampuni, zinawajibika kutoa gawio kwa wanahisa, Benki ya NMB ndiyo iliyoongoza kwa kutoa Shs. bilioni 54.5, ikifuatiwa na Twiga Minerals (ya ubia baina ya Serikali na Barrick Gold) iliyotoa Shs. bilioni 53.4, Airtel Tanzania (Shs. bilioni 40.8), Puma Energy (Shs. bilioni 12.2), na Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi kilitoa Shs. bilioni 10.2.

 

Licha ya kumkabidhi Msajili wa Hazina kuhakikisha anayasimamia Mashirika ya Umma na Taasisi kuleta mabadiliko chanya, Rais Samia alionya wale ambao watathubutu kumkera kwa kumkanyagia uchumi wake anaoupambania.

 

“Anayetaka kunikera anikanyagie uchumi wangu. Kwenye mageuzi haya wapo wengi watakaokanyagwa na kupiga kelele nyingi, lakini msikate tamaa, kachapeni kazi,” alisema.

 

Akaongeza kwamba, ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania. Jukumu hili la usimamizi liko chini ya Msajili wa Hazina.

Akayasihi mashirika ya Serikali kujiangalia upya katika utendaji kazi wao ili waweze kutoa gawio kwa Serikali.

 

Ni wazi kwamba, upokeaji gawio ni ishara kuwa mazingira yaliyowekwa yanafanya kazi na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufanya bishara na kupata faida.

Hapa Rais Samia alisisitiza kwamba, Serikali inaweka mazingira bora ya kufanya biashara, kutunga sera rafiki zinazohamasisha uwekezaji nchini kwa nia ya kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii.

 

Kimsingi, Msajili wa Hazina analo jukumu zito katika kusimamia mageuzi kwenye mashirika ya umma kwa sababu huo ndio wajibu wake mkubwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

 

Kifungu cha 8(f) cha Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina SURA 370, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 11(3) cha Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 vimeweka wajibu kwa Wakala wa Serikali, Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

 

Aidha, kifungu cha 7 cha Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257, pamoja na mambo mengine, kimeelekeza Mashirika ya Umma kujiendesha kwa misingi thabiti ya kibiashara na kupata rejesho la mtaji lisilopungua asilimia 5, na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

 

Halikadhalika, Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, kifungu cha 10(2)(i) kinatoa wajibu kwa Msajili wa Hazina kufuatilia na kuhakikisha michango na gawio kutoka katika Mashirika ya Umma inalipwa kwa wakati.

 

Na kifungu cha 10A(1) cha Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina kimeweka masharti ya mashirika ya umma kupunguza matumizi ambapo mashirika hayo yanatakiwa kutumia siyo zaidi ya asilimia 60 ya mapato baada ya kutoa gharama ya mishahara na bakaa inayopatikana baada ya matumizi hayo kuwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

 

Hali siyo nzuri

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema hali siyo nzuri kwa mashirika na taasisi za umma kwa sababu kati ya mashirika 304, ni mashirika 145 pekee yaliyotoa gawio la Shs. bilioni 637 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ilhali mashirika 159 hayakutoa kitu kabisa.

 

Akasema pia kwamba, mwaka 2023 jumla ya mashirika 109 ndiyo yaliyotoa gawio, hivyo mwaka huu kuna ongezeko la mashirika 36 huku akisisitiza kwamba, hali hiyo hairidhishi.

 

Hii ndiyo sababu ya msingi iliyomfanya Rais Samia kumkabidhi Msajili wa Hazina rungu la kusimamia maboresho kwenye Mashirika ya Umma kwa sababu, katika mashirika 304 ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Hazina, mashirika 248 Serikali ina hisa nyingi lakini mashirika 56 ambayo Serikali ina hisa chache ndiyo yaliyoongoza kwa kutoa gawio kubwa.

 

Mchechu atoa angalizo kwa mashirika ya umma kuhusu utoaji wa gawio ambapo alisema kampuni na mashirika 10 bora yaliyotoa gawio serikalini ni ambayo Serikali ina hisa chache.

 

Akasema mafanikio hayo ni somo ambalo Serikali ina kila sababu ya kujifunza namna taasisi zake zinavyoendeshwa kwa sababu uwekezaji wa Serikali katika kampuni na mashirika hayo ni Shs. 3 trilioni. Kwa ujumla, Serikali imewekeza Shs. 76 trilioni kwenye mashirika na taasisi mbalimbali.

 

Mchechu akasema, mwaka 2019/2020, 2020/2021, na 2021/2022 mashirika ya umma yalichangia Shs. 255 bilioni, Shs. 161 bilioni na Shs. 207 bilioni, mtawalia, huku kampuni na mashirika ambayo Serikali ina hisa chache yakichangia gawio dogo la Shs. 44 bilioni, Shs. 147 bilioni na Shs. 10 bilioni mtawalia.

 

Lakini akasema, kwa miaka miwili 2022/2023 na 2023/2024 gawio kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara lilikuwa Shs. 109 bilioni na Shs. 110 bilioni mtawalia; huku ambako Serikali ina hisa chache yakichangia Shs. 219 bilioni na Shs. 168 bilioni kwa kipindi hicho.

 

“Matokeo haya kwetu yanaleta fikra mchanganyiko, ni habari njema kwa kuwa inaonyesha uwezeshaji unaofanywa na Serikali kuendeleza mazingira wezeshi ya biashara, kampuni binafsi inapofanya kazi na kupata faida, mazingira ni mema,” akasema Mchechu.

 

Akasema, faida katika biashara ya sekta binafsi ni kipimajoto cha mafanikio ya Serikali kuboresha mazingira ya biashara na sera za kiuchumi huku akiwataka viongozi waliochaguliwa kuongoza mashirika ya umma kufanya vizuri zaidi kwa faida ya Taifa na wananchi.

 

“Kama tutazingatia Shs. 850 bilioni mwaka hadi mwaka inawezekana tukawa na furaha, lakini kama tutaangalia kiwango hiki tunachotoa sasa kwa malengo tuliyopatiwa tukiwa Arusha ya mapato yasiyo ya kikodi yafikie asilimia 10 ya kikodi tuko mbali sana, mwaka jana tulikuwa asilimia tatu na mwaka huu tupo asilimia tatu,” akasema.

 

Mchechu akasema ni lazima ukuaji uwe wa wastani wa asilimia kati ya 60 hadi 70 ili kufikia malengo ya mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 10.

“Hali si nzuri kwa sababu bado hatuendani na kasi na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo kwa kasi nchini, maendeleo yote yanategemea fedha, chanzo cha fedha ni vitu vitatu, Serikali kukopa, kukusanya kodi au kupata mapato yasiyo ya kikodi. Asilimia 90 ya mapato yasiyo ya kikodi hupatikana kupitia gawio,” akasema.

 

Mchechu alieleza baadhi ya mafanikio ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina imeyapata kwamba, imeendelea kushawishi kufanyika kwa mabadiliko katika sheria yake ili kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, muswada ambao ulipelekwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10, 2023.

 

“Ni wazi kuwa tunahitaji sheria inayojitosheleza itakayoweza kusaidia kuleta tija katika uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shs. 76 trilioni uliofanywa na Serikali kwa niaba ya Umma wa Watanzania,” akasema Mchechu.

 

Mchechu alisema, katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, Ofisi ya Msajili imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa.

 

Akasema, Ofisi imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika (Key Performance Indicators) vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina, vigezo ambavyo vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi.

 

“Tupo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti (dashboard) taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati (informed decision making) kwa mamlaka za uteuzi.

 

“Ofisi pia imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za uchumi; kwenye sekta ya madini kumekuwa na mzungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya kampuni, mathalani, tumeongeza hisa za serikali katika kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo.

 

“Pia tumekamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10,” akafafanua Mchechu.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema miongoni mwa mambo wanayosimamia ni mchango wa taasisi kwenye uchumi kuhakikisha unaongezeka na kupunguza mzigo kwa Serikali unaotokana na kuhudumia taasisi hizo.

 

“Hapa Rais ni pagumu pia kwa sababu ulituelekeza tufanye tathmini ya mashirika ya umma ili yale ambayo yamepitwa na wakati tukushauri uyafute na mengine tuyaunganishe, tumefanya kazi hiyo kwa awamu ya kwanza tunaenda kuunganisha mashirika 16 na mengine manne yanaenda kufutwa,” akaeleza Prof. Mkumbo.

 

Profesa Mkumbo akasema, hilo ni gumu kwa kuwa alinyooshewa vidole kuwa anakwenda kuua mashirika ya umma, lakini akasisitiza kuwa, mashirika yatakayounganishwa, wenyeviti wa bodi ama mmoja atabaki au wote wataondoka na haiwezekani wote wawili wafanye kazi.

 

“Mashirika hayo ndiyo yanafanya kazi na mashirika binafsi, hivyo kuwa na mashirika ambayo hayaangalii biashara vizuri, mazingira ya biashara yatakuwa magumu,” akasema.

 

Katika kuwapa morali, Rais Samia aliwataka wachape kazi na akahimiza viongozi wa mashirika, wakiwemo wenyeviti na wakurugenzi wa Bodi, kusimamia mashirika ili mwakani zipatikane fedha nyingi zaidi.

 

Akasema, licha ya mashirika mengi kutopeleka gawio serikalini, kuna mageuzi ambayo yanafanyika huko na akawaagiza Wenyeviti wa Bodi kuyasimamia mashirika hayo.

Akarudia onyo lake kwa viongozi wa Wizara wenye mashirika, kwamba waache kuagiza fedha kutoka kwenye mashirika hayo na kuwataka wawe wabunifu kuangalia vyanzo vya fedha ili wakuze mashirika hayo.

 

Akawataka kufanya kazi ili kukuza mashirika yao kutokana na serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao na si kubaki nyuma huku akisisitiza kwamba, mageuzi kwenye mashirika lazima yaendelee ili kuendelea kukuza uchumi ambapo nchi itafanyiwa tathmini ya uchumi wake ili kuingia uchumi wa kati.