Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Ofisi ya Msajili wa Hazina yakabidhi rasmi mashamba ya wanyamapori ya Lente, Loldebes na Amani, Arusha
02 Nov, 2023
Ofisi ya Msajili wa Hazina yakabidhi rasmi mashamba ya wanyamapori ya Lente, Loldebes na Amani, Arusha

Ofisi ya Msajili wa Hazina jana Oktoba 3, 2023 imekabidhi rasmi mashamba ya Wanyamapori ya Lente, Loldebes na Amani yaliyopo wilaya  ya Monduli Mkoani Arusha kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa utalii.

Mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe. Joshua Nassari ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano ya mashamba hayo iliyofanyika ndani ya eneo la mashamba  almaarufu “Makuyuni Wildlife Park” amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi yake ya kubadilisha matumizi ya mashamba kutoka kwenye shughuli za kilimo na kurasimisha ili yaweze  kutumika kwa shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa utalii.

Mhe. Nassari amesema maamuzi hayo  yanakwenda kufungua fursa nyingi zenye tija kwa wakazi wa Monduli kutokana na uwekezaji utakaofanywa na TAWA katika eneo hilo na kuitaka TAWA iliendeleze  eneo hilo kwa haraka kwakuwa ni eneo muhimu, lenye rasilimali nyingi na linafikika kirahisi.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen.(Mstaafu) Hamis Semfuko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuridhia TAWA ikabidhiwe mashamba hayo kwa ajili ya Uhifadhi na uendelezaji wa utalii

Aidha, Semfuko amesema kwakuwa eneo hilo lina fursa kubwa ya Utalii TAWA imelipa jina la kibiashara la “Makuyuni Wildlife Park” na kwamba maono ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA ni kuongeza mapato na kuimarisha Uhifadhi na italitumia eneo hilo kwa utalii wa picha na kwa kuanza itajenga miundombinu wezeshi ili kuwezesha shughuli za uhifadhi na Utalii kufanyika kikamilifu pamoja na kuvutia wawekezaji

Awali akielezea historia ya mashamba hayo, Mkurugenzi wa ubinafsishaji, ufuatiliaji na tathmini – Ofisi ya Msajili wa Hazina Mohamed Nyasama amesema mnamo tarehe 02 Juni, 2022 Msajili wa Hazina kupitia barua yake alikabidhi mashamba hayo kwa TAWA kwa ajili ya Usimamizi wa muda wakati wakisubiri maelekezo ya Mamlaka.

Ameongeza kuwa  tarehe 27 februari 2023 Mamlaka ilitoa maamuzi na kupitia barua ambayo iliandikwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya fedha ilitoa  maelekezo kuhusiana na matumizi ya eneo hilo na kupitia barua ya Katibu Mkuu kiongozi walitaarifiwa kuwa Mamlaka imeridhia mapendekezo ya kamati kuwa mashamba hayo ya Lente, Loldebes na Amani) yakabidhiwe rasmi kwa TAWA ili yatumike kwa ajili ya uhifadhi na uendelezaji wa utalii