Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Mradi wa Kabanga Nikeli mbioni kuanza
09 Jun, 2026
Mradi wa Kabanga Nikeli mbioni kuanza

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Mradi wa Kabanga Nikeli, ambao ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa na wa kimkakati katika sekta ya madini na viwanda nchini Tanzania, unakaribia kuanza kutekelezwa kufuatia maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika mazungumzo na maandalizi ya mradi huo.

 

Mradi huo wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni mbili (yapata Sh 5.2 trilioni), unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya madini na uongezaji thamani nchini, huku ukichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya viwanda, ajira na ukuaji wa uchumi.

 

Taarifa hiyo iliwasilishwa Jumatatu, Juni 8, 2026, na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, pamoja na Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Kabanga Nickel Limited na Lifezone Metals (NYSE: LZM), Bw. Keith Liddell.

 

Baada ya kikao hicho, viongozi hao walieleza kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa na kuthibitisha dhamira yao ya kuendelea kuusukuma mbele mradi huo kwa namna itakayoiwezesha Tanzania kunufaika kwa kiwango kikubwa zaidi.

 

Akizungumza baada ya kikao hicho, Bw. Mchechu alisema Mradi wa  Kabanga Nikeli ni uwekezaji wa mageuzi wenye uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya viwanda, uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi wa taifa.

 

Alisema msimamo wa Serikali umekuwa ni kuhakikisha shughuli za uongezaji thamani madini zinafanyika ndani ya Tanzania ili nchi iweze kupata manufaa makubwa zaidi kutokana na rasilimali zake za madini.

Bw. Mchechu alikiri kuwa mazungumzo ya miradi mikubwa ya aina hii huwa na changamoto nyingi na huhitaji muda, lakini akabainisha kuwa majadiliano ya hivi karibuni yamesaidia kutatua masuala kadhaa yaliyokuwa bado hayajakamilika na kuweka msingi mzuri wa utekelezaji unaokubalika kwa pande zote.

 

“Tumefanikiwa kuandaa muundo ambao Serikali na wawekezaji wote wanauridhia. Kwa sasa tunaendelea kukamilisha masuala yaliyosalia ili utekelezaji wa mradi uweze kuanza,” alisema.

 

Aliongeza kuwa wakati maandalizi ya upande wa mgodi yakiwa yamefikia hatua nzuri, juhudi za sasa zimeelekezwa katika kukamilisha mipango ya kiwanda cha kuchenjua madini na shughuli za uongezaji thamani ambazo ni sehemu muhimu ya mradi huo.

 

“Juhudi hizi zinaendana kikamilifu na maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ana shauku ya kuona mradi huu unatoka katika hatua ya mazungumzo na kuingia katika utekelezaji,” alisema.

 

Bw. Mchechu alisema mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa kupitia ushiriki wa wazawa, mapato ya kodi, gawio, uhamishaji wa teknolojia pamoja na maendeleo ya viwanda.

 

Kwa upande wake, Bw. Liddell alisema kikao chake na Mhe. Rais Samia kimebeba matumaini makubwa kwani Rais alithibitisha tena dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono mradi huo pamoja na jitihada za Serikali na wawekezaji za kuusogeza mbele.

 

“Ilikuwa heshima kubwa kukutana na Mheshimiwa Rais. Amethibitisha tena dhamira yake kwa mradi huu na kuunga mkono utekelezaji wake kwa kuzingatia mpango uliokubaliwa,” alisema.

 

Bw. Liddell alisema mazungumzo yao yalijikita katika kuusogeza mradi kwenye hatua ya maendeleo na utekelezaji huku yakihakikisha kuwa shughuli za uongezaji thamani na uchakataji wa madini zinabaki kuwa sehemu muhimu ya mradi.

 

Alisema pande zote zimefikia maelewano kuhusu muundo wa mradi huo, hususan namna shughuli za uongezaji thamani zitakavyofanyika nchini Tanzania kwa manufaa ya taifa na wadau wote.

 

Akitoa ujumbe kwa wadau, wawekezaji na wananchi wanaofuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo, Bw. Liddell alisema ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wake.

 

“Mgodi unakuja. Uongezaji thamani unakuja. Muwe na uhakika kwamba tunafanya kazi kwa karibu na Timu Tanzania ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa haraka iwezekanavyo,” alisema.

 

Mradi wa Kabanga Nikeli unatarajiwa kuiweka Tanzania katika nafasi muhimu katika mnyororo wa kimataifa wa usambazaji wa madini muhimu kwa maendeleo ya teknolojia na viwanda, huku ukihakikisha kuwa thamani kubwa zaidi ya rasilimali hizo inaongezwa ndani ya nchi.

 

Mradi huo pia unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ajenda ya taifa ya maendeleo ya viwanda kupitia uanzishaji wa ajira, ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa madini, uhamishaji wa teknolojia na kuongeza mapato ya muda mrefu yatokanayo na kodi, gawio na shughuli nyingine za kiuchumi.