Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Serikali kupitia upya mikataba yote ya madini
17 Oct, 2024
Serikali kupitia upya mikataba yote ya madini

 

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha serikali inaendelea kuongeza hisa 'free-carried interest shares' kwenye kampuni za madini, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza hatua za awali kupitia mikataba yote ambayo serikali imeingia na kampuni zote za madini.

 

Hayo yalisemwa Alhamisi (Oktoba 17) na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, siku chache baada ya serikali kuongeza hisa zake katika kampuni ya madini ya SOTTA kutoka asilimia 16 hadi 20.

 

Hii ni kampuni ya kwanza ya madini kwa serikali kuongeza hisa inazomiliki, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, kutoka asilimia 16 hadi kufikia asilimia 20.

 

Sasa serikali inaona ni muda muafaka wa kampuni zote za madini kuzungungumza lugha moja, nayo ni, ‘kuiongezea hisa serikali’.

 

“Tunapitia mikataba ya madini ili kubaini mapungufu na kuyatolea maoni kwa ajili ya marekebisho,” alisema Bw. Mchechu.

         

Moja kati ya mapungufu, alifafanua, ni la umiliki wa asilimia 16 ambapo sheria haijasema ni 16, bali ni angalau 16.

 

Tafsiri yake ni kuwa inaweza ikawa ni asilimia 16 au zaidi, lakini kampuni nyingi zimekuwa zikisimamia kwenya asilimia 16.

 

Afisa Mkuu wa Fedha wa Kampuni ya SOTTA, Bw Isaac Lupokela, alisema kuongezeka kwa hisa za serikali katika kampuni ya SOTTA kumechagizwa na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara ya madini.

 

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana wakati wa kilele cha maonesha ya saba ya Teknolojia na Uwekezaji katika Madini.

 

Bw. Lupokela alikuwa anatoa maelezo kwa Mhe. Rais Dk. Samia, kuhusu uwekezaji wa kampuni ya SOTTA inayotarajia kuwekeza kwenye mgodi mkubwa wa dhahabu wa Nyazaga kiasi cha $500 milioni (yapata Sh1.4 tirioni).

 

       Habari hii imeandaliwa na

       Ofisi ya Msajili wa Hazina.