Hisa za serikali Kampuni ya SOTTA zafikia asilimia 20

Dar es Salaam. Ikiwa ni matunda ya sera nzuri za uwekezaji Tanzania chini ya Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali imeongeza umilika wa hisa katika kampuni ya madini ya SOTTA hadi kufikia asilimia 20.
Hii ni kampuni ya kwanza ya madini kwa serikali kuongeza hisa inazomiliki, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, kutoka asilimia 16 hadi kufikia asilimia 20.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema Alhamisi (Oktoba 17) kuwa ongezeko la hisa hizo ni matokeo ya mazungumzo mazuri kati ya serikali, kupitia Ofisi yake, na mwekezaji mwenza, kampuni mama ya Perseus Mining Limited ya Austraria.
“Ongezeko hilo litapelekea kuongezeka kwa gawio la faida (dividend) na faida zingine za kiuchumi zinazotokana na mradi,” alisema Bw. Mchechu.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Fedha wa Kampuni ya SOTTA, Bw Isaac Lupokela, alisema kuongezeka kwa hisa za serikali kumechagizwa na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara ya Madini.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jana wakati wa kilele cha maonesha ya saba ya Teknolojia na Uwekezaji katika Madini
Bw. Lupokela alikuwa anatoa maelezo kwa Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhusu uwekezaji wa kampuni ya SOTTA inayotarajia kuwekeza kwenye mgodi mkubwa wa dhahabu wa Nyazaga kiasi cha $500 milioni (yapata Sh1.4 tirioni).
Mgodi huo, alieleza, utakaojengwa kwa takribani miaka 15, unatarajiwa kutoa ajira kwa watanzania 1,500.
“Uwekezaji wetu ni kielelezo cha sera nzuri za Tanzania chini ya ya Mhe. Rais, Dr. Samia Suluhu Hassan, zenye mlengo wa kuvutia wawekezaji,” alisema Bw. Lupokela.
Umri wa kampuni hii, ambayo inatarajia kurudisha mtaji baada ya miaka mitatu, ni miaka 15.
“Mpaka sasa Taifa limeanza kunufaika na mgodi huu kupitia ajira ambazo tayari tumetoa, na kodi ya mapato yaani ‘capital gain tax’,” alisema Bw. Lupokela.
Alifafanua kuwa kipindi walipokuwa wanaleta mtaji mwezi wa nne na watano mwaka huu, kiasi cha $16 milioni (yapata Sh43.6 bilioni) kilitolewa kwa Serikali kama kodi ya mapato.
“Hii ni ishara nzuri ya mwelekeo juu ya uwekezaji na mgodi huu,” alielezea matumaini yake.
Tayari kampuni hiyo imelipa fidia zadi ya asilimia 94 kwa wale waliochagua kulipwa pesa na asilimia zilizobaki ni wale ambao ardhi yao ina mgogoro.
Kwa sasa, Bw. Lupokela alisema wanaendelea kutoa mikataba mikubwa kwa kandarasi kwaajili ya ujenzi wa mgodi.
“Mhe. Rais tunakuthibitishia kwamba chini ya uongozi wako mgodi utaanza, ili tuweze kujivunia sera nzuri za uwekezaji na kupata manufaa kama Taifa kwasababu ya mgodi huu wa Nyanzaga,” alihitimisha.
Habari hii imeandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina.