Serikali: Mafunzo yapewe kipaumbele
Kibaha, Pwani. Serikali imezitaka taasisi za umma kuhakikisha zinatoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wake ili kuwapatia maarifa na ujuzi kwa lengo la kuongeza ufanisi wao.
Agizo hilo lilitolewa jana Kibaha, Pwani na Bw. Xavier Mrope Daudi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais---Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora wakati wa kufunga mafunzo elekezi kwa wakuu wapya wa taasisi za umma.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi, yalilenga kuwajengea uwezo watendaji wakuu wapya ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina imeonesha njia, tunahitaji kujifunza. Jengeni utamaduni wa kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wenu,” alisema Bw. Daudi.
Aliongeza: “Kuwapa watumishi wetu maarifa na ujuzi stahiki itakuwa chachu kwa maendeleo ya taasisi zetu za umma.”
Aidha, aliwataka wakuu hao wa taasisi kwenda kuwafundisha wasaidizi wao yale waliyofundishwa kwa siku tatu na wataalamu nguli kutoka sekta ya umma na binafsi.
Kwa kufanya hivyo, aliongeza Bw. Daudi, wakuu hao wa taasisi watasimamia kwa ufanisi taasisi wanazoziongoza.
“Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha pesa kwenye taasisi za umma na ni kwa muktadha huo, inahitaji kuona mnasimamia vizuri taasisi hizo,” alisema.
Katika nchi hii kuna taasisi, mashirika ya umma na wakala wa serikali 309 ambapo uwekezaji wake ni Sh75.8 tirioni, kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Tunataka muongeze ufanisi katika kuendesha taasisi za umma. Tunataka mpunguze utegemezi kwa serikali. Tunataka muongeze mchango wenu kwa mfuko mkuu wa serikali,” alisisitiza Bw. Daudi.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, alisema muda wote milango ya ofisi yake iko wazi kwaajili ya kuzisaidia taasisi za umma.
“Tumieni Ofisi ya Msajili wa Hazina. Sisi ni kiungo chenu cha kufika kule mnakotaka kwenda,” alisema Bw. Mchechu.
Alienda mbali kwa kuongeza: “Tutaendelea kutengeneza mazingira rafiki yatakayoleta matokeo chanya katika taasisi za umma.”
Alisema ofisi yake itaendelea kufanya mageuzi katika taasisi za umma ili yajiendeshe kiufanisi na kupunguza au kuachana na utegemezi kutoka kwa serikali kuu.
“Lazima tufanye mabadiliko licha ya kuwa si rahisi. Lazima tufanye mabadiliko kwa kuwa hayazuiliki,” alihitimisha Bw. Mchechu.
Habari hii imeandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina.