Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

TADB kutoa gawio la Sh5.58 bilioni kwa Serikali
15 May, 2026
TADB kutoa gawio la Sh5.58 bilioni kwa Serikali

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza kutoa gawio la Sh8.38 bilioni kwa Serikali katika mwaka wa fedha 2025/26, imebainishwa Ijumaa, Mei 15, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wanahisa wa benki hiyo.

 

Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 50.2 ikilinganishwa na kiasi cha Sh5.58 bilioni kilichotolewa katika mwaka wa fedha 2024/25.

 

Akizungumza katika mkutano huo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

 

Amesema Serikali itaendelea kuiunga mkono TADB kutokana na umuhimu wake wa kimkakati katika kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

 

Amesema hadi sasa Serikali imewekeza jumla ya Sh452.37 bilioni kama mtaji wa Benki hiyo, huku akisisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha sekta ya kilimo inaendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na ajira nchini.

 

Aidha, Msajili wa Hazina amepongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa TADB kwa kuendelea kuimarisha utendaji wa Benki na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unakuwa na tija.

 

 

Naye Mkrugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege pamoja na kueleza mafanikio ya Benki kwa mwaka ulioishia Desemba 2025, pia ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiunga mkono na kuhakikisha inatimiza malengo yaliyokusudiwa.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika mkutano huo na Mkrugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, TADB ilirekodi faida kabla ya kodi ya Sh35.45 bilioni mwaka 2025 ikilinganishwa na Sh24.68 bilioni mwaka 2024.

 

Vilevile, aliongeza Bw. Nyabundege, faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 50 hadi kufikia Sh27.94 bilioni.

 

Aliendelea kusema kuwa katika kipindi hicho kitabu cha mikopo kiliongezeka kutoka Sh534.16 bilioni mwaka 2024 hadi Sh806.75 bilioni mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 51.

 

Thamani ya mali za Benki pia iliongezeka kwa asilimia 41 na kufikia Sh1.3 trilioni.

 

“Mafanikio hayo yamechagizwa na upatikanaji wa rasilimali fedha, ongezeko la mtaji, mazingira wezeshi ya utendaji wa TADB na uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Bw. Nyabundege.

 

Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kusimamia kwa karibu uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa ufanisi, kuleta tija kwa Taifa na kuchangia maendeleo ya wananchi.