Watumishi wa Umma waaswa kushiriki Uchaguzi wa Oktoba 29
Na Mwandishi wa OMH
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imetoa wito kwa watumishi wote wa umma walioko katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Ofisi imesisitiza kuwa ushiriki wa watumishi wa umma ni sehemu muhimu ya kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na amani ya nchi — nguzo kuu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu unaokadiriwa kufikia $1 trilioni ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jumatatu, Oktoba 27, 2025, jijini Dar es Salaam, Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, alisema watumishi wa umma wana nafasi ya kipekee katika kuhakikisha dira ya maendeleo ya Taifa inatimia, kwa kuwa wao ndio watendaji wakuu wa sera na mipango ya Serikali.
“Ushiriki wa watumishi wa umma katika uchaguzi ni zaidi ya kutekeleza haki ya kikatiba. Ni tendo la kizalendo linaloimarisha misingi ya utawala bora na kuonesha dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi na uchumi imara,” alisema Bi. Mauki.
Aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka dira thabiti ya maendeleo inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi unaotegemea uwazi, uadilifu na ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya Taifa.
Hivyo, kushiriki kwa watumishi wa umma katika uchaguzi ni mchango wa moja kwa moja katika kuhakikisha uendelevu wa dira hiyo, kwani viongozi wanaochaguliwa kupitia demokrasia ndio wanaotekeleza mipango ya maendeleo kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Bi. Mauki, kupiga kura ni wajibu wa kiraia unaoimarisha umoja, uthabiti wa Taifa na uwajibikaji.
Kupiga kura kunawawezesha wananchi — wakiwemo watumishi wa umma — kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji, ambao watasimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa tija.
Aidha, Bi. Mauki alibainisha kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi.
Kupitia jukumu hilo, OMH imeendelea kuhimiza ustawi wa rasilimaliwatu, uwajibikaji wa viongozi na utendaji bora wa taasisi za umma kama sehemu ya msingi wa kujenga uchumi imara na endelevu.
“Ushiriki mkubwa wa watumishi wa umma katika uchaguzi unaonesha mfano wa uzalendo, nidhamu ya kitaifa na uelewa wa majukumu ya kikatiba,” alisema.
Aliongeza: Huu ndio msingi wa utumishi bora wa umma unaounga mkono safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050,” alisisitiza Bi. Mauki.