Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Wakurugenzi wa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kukutana Machi 16
27 Feb, 2026
Wakurugenzi wa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kukutana Machi 16

Na Mwandishi wa OMH

 

Dar es Salaam. Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache (Minority Interest Forum – MIF 2026) linatarajiwa kufanyika Machi 16 hadi 18 katika Ukumbi wa PAPU, jijini Arusha.

 

Mgeni rasmi wa mkutano huo, unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), anatarajiwa kuwa Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji.

 

Mkutano huo unaowaleta pamoja zaidi ya Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu 150 kutoka kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki chini ya asilimia 51 ya hisa, unalenga kuimarisha uongozi wa kimkakati katika kampuni ambazo Serikali ina uwekezaji wa hisa chache.

 

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kutoka Ufuatiliaji wa Kawaida hadi Uongozi wa Kimkakati Unaotazama Mbele,” ikilenga kuhamasisha mabadiliko kutoka uongozi wa kufuatilia tu utendaji kwenda uongozi bunifu, unaotambua vihatarishi na fursa mapema na kujibu kwa haraka mabadiliko ya kiuchumi na kibiashara.

 

Kupitia mkutano huo, washiriki watajadili namna ya kuimarisha utawala unaotazama mbele na unaozingatia vihatarishi vinavyoibuka katika mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kasi.

 

Pia mjadala utaangazia umuhimu wa ubunifu na ushindani endelevu, athari za siasa na uchumi wa kimataifa, changamoto za usalama wa mitandao na mtikisiko wa masoko ya fedha na bidhaa.

 

Aidha, mkutano utatathmini jinsi mikakati ya taasisi inavyoweza kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mipango ya muda wa kati, sambamba na matumizi ya teknolojia katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora.

 

Katika kuimarisha maamuzi ya uwekezaji, washiriki pia watapata fursa ya kujadili matumizi ya uchambuzi wa taarifa za kiuchumi na ushindani (economic and competitive intelligence) kama nyenzo ya kuongeza ufanisi na tija katika kampuni hizo.

 

Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache ni zile za kibiashara ambazo Serikali inamiliki chini ya asilimia 51 ya hisa.

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma, Sura ya 257, taasisi ambazo Serikali inamiliki asilimia 51 au zaidi hutambuliwa kama Mashirika au Taasisi za Umma.

 

Hadi Juni 30, 2025, kulikuwa na Taasisi za Umma 252 na Kampuni zenye Hisa Chache 56, hivyo kufanya jumla ya taasisi 308 zinazosimamiwa na OMH.

 

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kampuni hizo imeongezeka kutoka Sh821.51 bilioni mwaka 2020 hadi Sh1.94 trilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 136.

 

Mapato ghafi yameongezeka kutoka Sh6.81 trilioni hadi Sh10.74 trilioni, huku faida ikiongezeka kutoka Sh1.79 trilioni hadi Sh1.95 trilioni.

 

Katika kipindi hicho, kampuni hizo zimechangia takribani Sh3.67 trilioni kama kodi ya mapato ya kampuni, wakati gawio kwa Serikali likiongezeka kutoka Sh58.26 bilioni hadi Sh266.52 bilioni.

 

Ukuaji huo unaakisi mchango wa kampuni zenye hisa chache katika kukuza mapato ya Serikali, ajira, ujuzi wa Watanzania na maendeleo ya sekta mbalimbali za kimkakati.

 

Mwelekeo huo unaendana na maono ya Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kujenga uchumi shindani na jumuishi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.