Agizo la Rais, Dkt John Magufuli la kuzitaka taasisi, kampuni na mashirika ya umma kuwa yametoa gawio, michango na ziada ndani ya siku 60 kuanzia Novemba 24, mwaka huu, tayari taasisi nne zimetekeleza agizo hilo ndani ya saa 24 kwa kutoa jumla ya Sh bilioni 2.75.

Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesisitiza kuwa hatakuwa na huruma na taasisi zitakazoshindwa kutii agizo hilo.

Taasisi ambazo zimetekeleza agizo hilo la kutoa gawio, michango na ziada ni Self Microfinance iliyotoa Sh milioni 200, Shirika la Posta Tanzania (TPC) iliyotoa Sh milioni 350, Shirika la Reli Tanzania (TRC) iliyotoa Sh bilioni 1 wakati Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiongoza kwa taasisi ambazo zilitoa fedha hizo kwa kutoa Sh bilioni 1.2.

Akizungumza baada ya kupokea hundi ya mfano hivi karibuni, Dk Mpango alisema, “Kama mnakumbuka, jana (Jumapili Novemba 24, 2019) Rais alinipa kazi ya kuhakikisha taasisi hizo zitoa gawio, kinyume chake mwenyekiti wa bodi, wajumbe wake na wakuu wa taasisi wajue wamejitoa, na alisema damu yao iwe juu yangu.

“Nitasimamia maagizo ya rais, kwa atakayekaidi nitashusha panga bila huruma wala woga na bila kupepesa macho.

Hizi fedha zinazokusanywa si za Rais Magufuli, au za Dk Mpango ni fedha za wananchi ambao fedha zao zimewekezwa huko, kwa kutoa gawio ni ushahidi kuwa mnazifanyia kazi fedha zao,” alisema Dk Mpango.

Aidha, amewataka wenyeviti wa bodi na wajumbe wao na wakuu wa taasisi ambazo hajatoa gawio, michango na ziada kutumia siku 59 zilizobaki kufanya hivyo ili kukwepa mkono wake.

Amesema kazi yake kuu ni kuhakikisha anakusanya mapato ya kodi na yasiona kodi, mikopo na misaada.

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema baada ya juzi kupewa agizo hilo na Rais, siku hiyo hiyo aliziandikia taasisi, mashirika na kampuni ambazo hazikuwa zimetoa gawio.

Alisema kwa kampuni hizo kuongezeka kunafanya sasa taasisi, kampuni na mashirika 83 kuwa yametoa fedha hizo kwa serikali kati ya 266.