Hatua iliyochukuliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ya kuhakiki mali za serikali, imezaa matunda na kufanikisha kurejeshwa serikalini kwa kampuni mbili na kuongeza hisa katika kampuni ya Airtel na UDART.

Wakati uhakiki ukiokoa mali na kuongeza hisa za Serikali, kampuni ambazo serikali ina hisa, taasisi na mashirika ya umma zimetoa gawio na mchango wa jumla ya Sh trilioni 1.05 katika Mwaka wa Fedha wa 2018/19.

Hayo yamebainishwa na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka hivi karibuni wakati wa hafla ya kukabidhi gawio na michango kutoka kampuni, taasisi na mashirika ya umma 79 ambapo Rais Dkt John Magufuli alikuwa mgeni rasmi katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Mbuttuka alisema katika kutekeleza maagizo ya rais, ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango wamefanya uhakiki wa mali za serikai katika mikoa 10, idadi ya mali 531 zilikuwa zimetambuliwa sambamba na uwepo kwa kampuni mbili ambazo zilikuwa hazijulikanani kama ni za serikali.

Amezitaja kampuni hizo kuwa ni Songwe Water Company Limited ambayo serikali inamiliki kwa asilimia 100 na Liquid Storage Company Ltd ambayo serikali inamiliki kwa asilimia 40.

Alitaja mali zingine zilizorejeshwa kuwa ni majengo 337, viwanja 140, mashamba 10, maghala 41.

Mbuttuka alisema pia hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, ofisi yake imerejesha viwanda 31 vilivyothibitika kutofanya kazi na taratibu za kisheria zinaendelea katika hatua mbalimbali.

Kuhusu ongezeko la hisa, alisema wamefanya mazungumzo na Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 49 na Kampuni ya Usafirishaji Jiji la Dar es Salaam, UDART kutoka asilimia 49 hadi kufikia asilimia 85.

Alisema kumekuwapo na ongezeko la mapato ukilinganisha na mwaka uliopita kulikochangiwa na kuimarisha makusanyo, kupunguza matumizi yasiyo na tija, ukusanyaji wa maduhuli kwa mfumo wa kieletroniki, udhibiti wa matumizi na kuongeza usimamizi wa mashirika ya umma na kampuni zinazomilikiwa kwa hisa chache na serikali.

Alisema kampuni na mashirika 40 kati ya 81 yaliyopaswa kutoa gawio yameshindwa kutokana na kujiendesha kwa hasara au kuwa na mtaji mdogo.

Akizungumza urekebishaji wa mashirika na kampuni yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajii wa Hazina, Mbuttuka alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, mashirika 15 yaliunganishwa na kuwa mashirika sita na shirika moja lilitenganishwa na kuwa mashirika mawili.

Alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara yaFedha na Mipango pamoja na ESRF inaendelea kufanya tathmini ya kina kwa mashirika yote ya biashara kwa lengo la kubaini hatua stahiki za kuchukua ili kuboresha utendaji kazi wake.

Aidha, alisema pamoja na mafanikio hayo bado wanakabiliwa na changamoto ambazo zikipata ufumbuzi inaweza kuboresha zaidi ukusanyaji wa mapato.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mfumo hafifu wa Tekn0olojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa utoaji taarifa na ufuatiliaji, changamoto za Sheria ya Msajili wa Hazina, ongezeko la mahitaji ya watumishi wenye utaalamu na uzoefu wakazi, na kukosekana kwa Mfuko wa Fedha za Uwekezaji.

Taasisi zilitoa gawio na michango ni TPA, TCRA, NEMC, SMSI, TBA, TAWA, Temesa, TPRI, Bodi ya Sukari, Wakala wa Mbolea, Dawasa, TIRA, IFM, NIDA, TIA, TAA, Brela, FCC, Wakala wa Vipimo, OSHA, LATRA, Ewura, TCAA, TASAC, TMDA, TBS, Hifadhi ya Ngongoro, Tanapa, TFS, TPDC, TCRA, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha.

Nyingine ni NARCO, AICC, TANLAKE, UTT, TCC, NHC, KADCO, TPB, SUMA JKT, Kilombero Sugar, NMB, NBC, TIPPER, Puma Energy, Tanganyika Plantation, Sukari Moshi, CRDB, TANTRED, Stamico, Tanesco na ALAF.

Aidha, siku moja baada ya ghafla ya gawio, taasisi nyingine nne kati ya 187 zilitii agizo la Rais Magufuli la kutaka kutoa gawio ndani ya siku 60. Nne zilizowahi agizo ka Rais Magufuli ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Posta na Kampuni ya Self Microfinance.