Na Mwandishi Maalumu, Dodoma

SERIKALI imewaagiza Maafisa Masuuli wote wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha kuwa, mpango wa bajeti kwa mwaka 2021/22 unaandaliwa na kuwasilishwa kupitia mfumo mpya wa uandaaji wa bajeti (PlanRep).

Akizungumza katika uzinduzi wa mfumo wa uandaaji wa bajeti jijini Dodoma hivi karibuni, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo amemuelekeza Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kutochambua bajeti yoyote itayowasilishwa nje ya mfumo huu.

Amempongeza Msajili wa Hazina akisema kuwa utekelezaji wa mfumo huo ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na ofisi yake katika kuimarisha usimamizi wa fedha za umma katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma ikiwa ni pamoja na kuziba mianya inayosababisha Serikali kukosa mapato.

Aidha, aliwashukuru wadau wa maendeleo wanaofadhili Mradi wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) kwa kuwezesha kifedha ujengaji wa mfumo huo na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali katika kuimarisha maendeleo ya nchi yetu.

“Aidha nawapongeza kwa dhati vijana wetu, Watanzania wenzetu, ndani ya Serikali kwa weledi wao na jitihada zao zilizosababisha kufanikisha kujenga “customization” ya Mfumo huu, hongereni sana. Mwisho kabisa, hatuna budi kushukuru Serikali ya Awamu ya Tano, kwani mafanikio yote haya yamewezekana chini ya uongozi wake thabiti na imara,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Ameongeza kuwa ili kuwezesha ufanisi katika usimamizi wa mali za umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina inahitaji pamoja na mambo mengine kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki itakayorahisisha usimamizi wa rasilimali hizo.

Amesema uwepo wa mifumo hiyo utapunguza upotevu wa mapato, kuimarisha na kuchochea uwajibikaji, kuimarisha uchambuzi wa bajeti na ufuatiliaji na hatimaye kuongeza mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

“Nafahamu, ofisi yako haikuwa na mfumo ambao ungeiwezesha kufuatilia utekelezaji wa bajeti za Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma. Hivyo basi, mfumo huu utakuwa kitendea kazi muhimu cha ofisi yako, na naamini hata Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuu zitaweza kutumia mfumo na kuweza kuokoa gharama ambazo zinalipwa watoa huduma kwa ajili ya mfumo wa kibajeti,” alifafanua.

Amefafanua kuwa kufikia mwezi Juni mwaka 2019, Serikali ilikuwa imewekeza katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache zipatazo 266 zenye uwekezaji wa kiasi cha shilingi trilioni 59.6.

“Mashirika haya ni mengi na uwekezaji huu ni mkubwa na unahitaji usimamizi madhubuti utakaowezesha ongezeko la tija katika ukuzaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi,” alieleza.

Ameeleza furaha yake baada ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kujenga mfumo wa bajeti utakaotumika katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, akisema utakuja kuunganishwa na Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) na kuwezesha kudhibiti matumizi ya fedha za umma nje ya mipango na bajeti iliyoidhinishwa.

Awali, akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango kufungua mafunzo hayo, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina ikishirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango katika mwaka wa fedha 2019/20 ilianzisha mradi wa kusimika mfumo wa uandaaji na uwasilishaji wa bajeti kieletroniki uitwao PlanRep utakaotumika katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma.

Mbuttuka alisema mfumo huu wa bajeti tayari ulishaanza kutumika na Mamlaka za Serikali za Mitaa tangu mwaka 2017/18, na ofisi yake iliamua kuuboresha ili uweze kutumika na kila Taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Ameeleza kuwa mfumo huu wa PlanRep umejengwa na wataalamu wa ndani kwa kuzingatia matumizi sahihi ya takwimu za kifedha za Serikali (Government Financial Statistic- GFSM-2014), Chati ya akaunti (Chart of Account) iliyohuishwa, Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Taasisi, na mahitaji mengine mahususi ya Serikali.

Amesema kuwa katika hatua za ujenzi wa mfumo huo, jumla ya taasisi 32 zilialikwa na kufanya majaribio (User Acceptance Test), ambazo Taasisi na Mashirika hayo yalijumuisha yale yanayofanya biashara, huduma na ya udhibiti.

Mbuttuka amesema kuwa uwepo wa mfumo huu utasaidia kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma katika Mashirika na Taasisi za Umma pamoja na upatikanaji wa taarifa za uhakika na kwa wakati; kupunguza gharama kubwa za fedha za umma katika ununuzi, uundaji, usimikaji, uendeshaji na usimamizi wa mifumo hiyo.

Pia kupunguza utitiri wa mifumo ya kibajeti ya kieletroniki iliyoanzishwa bila kupata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni msimamizi mkuu wa fedha na mali za umma.

“Ndugu Mgeni Rasmi, inategemewa kuwa, uwepo wa mfumo huu utasaidia sana kuongeza ufanisi na tija katika usimamizi na ufuatiliaji wa uwekezaji wa Serikali katika Taasisi, kuboresha utendaji kazi wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza makusanyo ya serikali kutoka katika vyanzo vyake visivyo vya kodi,” alieleza.

Ameeleza kuwa pamoja na Mfumo huu uliozinduliwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina pia imeendelea na juhudi za kuimarisha utendaji kwa njia ya kielektroniki ambapo imetengeneza na inaendelea na utengenezaji wa Mifumo  mbalimbali ikiwemo Mfumo wa ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa za fedha (Financial Analysis and Reporting System), Mfumo wa Bodi za Wakururugenzi (OTR-MIS) na Mfumo wa Ufuatiliaji mali za Serikali (GIS/BIS).

Mafunzo hayo yatashirikisha washiriki 944 kutoka Taasisi na Mashirika yote 236 yaliyoko chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Mafunzo haya yanafanyika katika vituo vitatu tofauti ambavyo ni Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

ENDS