Na Mwandishi Maalumu, Arusha

SERIKALI imezindua mfumo mpya wa ufuatiliaji  na utekelezaji  wa mapendekezo  ya hoja za ukaguzi (GARI-ITS)  kwa Wakala wa Serikali, Taasisi na Mashirika ya  Umma ili kuimarisha udhibiti na usimamizi wa fedha za umma .

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya mfumo huo leo, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji, Ufuatiliaji na Tathmini katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama aliyemwakilisha Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka, alisema mfumo huo unatarajiwa kuimarisha mifumo ya ndani ya udhibiti na usimamizi madhubuti ya fedha za umma katika Wakala za serikali,taasisi na mashirika ya Umma.

“Ofisi yangu ilibaini uwepo wa wingi wa hoja za ukaguzi hasa kutoka Ukaguzi wa Ndani, Ukaguzi wa Nje (CAG) na maagizo yanayotolewa na Kamati za Kudumu za Bunge,” alisema Nyasama aliyesoma hotuba ya Msajili wa Hazina.

Katika hotuba hiyo, Msajili wa Hazina amewataka watendaji wakuu wa Wakala wa Serikali na Mashirika ya Umma kusimamia vyema na  kudhibiti fedha za Umma.

Alisema serikali inataka kunufaika na utekelezaji  wake uliofanyika katika taasisi ,Wakala na mashirika ya umma ili kuchangia  ukuaji wa mapato na hivyo kutoka huduma bora  kwa wananchi .

Awali, Mkaguzi Mkuu wa Ndani katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Magdalena Kirumba alisema wakaguzi wa ndani wamejipanga kutumia mfumo huo, kwani utaongeza ufanisi wa kazi.

Alisema mfumo huo utasaidia taasisi kuwasilisha taarifa za ukaguzi za kila robo mwaka na taarifa za mwaka  kwa wakati.

Wakaguzi wa ndani 472 kutoka taasisi za umma na mashirika ya umma 236 watajengewa uwezo juu ya mfumo huo mpya.

Mwisho