Na Mwandishi Maalumu

 

SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, imetangaza kuuza kwa njia ya zabuni mali za viwanda sita vinavyomilikiwa na Serikali.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya waliokuwa wawekezaji katika viwanda hivyokukiuka masharti ya uwekezaji, hivyo kurejeshwa serikali ambako sasa zinatafutiwa wawekezaji wapya wenye nia ya dhati na uwezo wa kuviendeleza ili viweze kukidhi dhamira ya serikali ya kuhakikisha vinaleta tija kwa taifa.

 

Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto kupitia tangazo la Ofisi hiyo katika vyombo vya habari na pia mitandao ya kijamii ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

 

Kwa mujibu wa tangazo hilo, viwanda ambavyo mali zake zimewekwa sokoni ni pamoja na Kiwanda cha kukoboa Mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Company Ltd kilichopo mkoani Kilimanjaro na Polysacks Company Limited cha Dar es Salaam.

 

Vingine ni NMC Mzizima cha jijini Dar es Salaam ambacho ni mahsusi kwa usagaji wa nafaka hasa mahindi. Pia vimo NMC Isaka cha Shinyanga na NMC Tabora cha mkoani Tabora vinavyojihusisha na ukoboaji wa mpunga.

 

Kiwanda kingine ni cha kutengeneza dawa za kuua wadudu cha Pesticides Manufacturers Limited         kilichopo mkoani Kilimanjaro.

 

Kwa mujibu wa tangazo hilo ambalo pia linapatikana www.tro.go.tz, twitter@MsajiliHazina, Instagram; @ofisi_ya_msajili_wa_hazina na facebook.com/ofisiyamsajilihazina, Ofisi ya Msajili wa Hazina itapokea maombi ya wanunuzi kwa muda wa wiki mbili kuanzia Februari 17, mwaka huu.