SIKU chache baada ya kununua shamba lenye ukubwa wa hekta 5,818 kutoka kwa mwekezaji aliyeshindwa kuliendesha na kulipa madeni ya mikopo, Serikali amelikabidhi shamba hilo kwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT) kwa lengo la kulisimamia wakati ikiangalia namna bora ya kuliendeleza.

 

Serikali ilinunua shamba hilo lililopo Mngeta, Kilombero mkoani Morogoro baada ya kushinda zabuni iliyoendeshwa na Mfilisi (Msimamizi wa Muda), Silvanus Mlola aliyewekwa na Benki ya NMB iliyokuwa inamdai mwekezaji, Kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL).

 

Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika shambani hapo jana, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto alisema shamba hilo linakadiriwa kuwa na mali zenye thamani ya Sh Bilioni  152 na hivyo kulifanya  kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 

“Ni dhahiri kuwa uwekezaji huu ni mkubwa na Serikali inahitaji kupata mapato kutoka uwekezaji huu thabiti na endelevu. Ni ukweli usiopingika kuwa wananchi wanaozunguka eneo hili watakuwa wanufaika wa kwanza wa mradi huu, na hivyo ni mategemeo ya Serikali kuwa SUMA JKT itafanya kazi kwa bidii katika kuendeleza mradi huu ili kutimiza lengo la Serikali.

 

“Hatutegemei kuona shamba linadorora na kurudi kule tulipolitoa, zaidi tunatazamia muendelee kuboresha miundombinu na shamba lizalishe, muimarishe ulinzi kwenye mipaka inayozunguka shamba ili kuepusha uvamizi na migogoro ya ardhi na wananchi,” alisema Mgonya.

 

Baada ya makabidhiano hayo, Mgonya ameielekeza SUMA JKT kuandaa Mpango wa Biashara utakaoonesha nia na mikakati yao, ili uweze kuchambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

 

Aidha, ili kulifanya shamba kujiendesha kwa tija, amesema baada ya uchambuzi wa mpango wa biashara na kubaini unafaa, Mamlaka inaweza kushauriwa kuundwa kwa kampuni tanzu chini ya SUMA JKT ambapo Serikali kupitia Msajili wa Hazina itakuwa na hisa kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa shamba hilo.

 

“Lengo ni kutaka kuona kwa pamoja tunafikia malengo na matarajio ya Serikali katika uwekezaji huu,” alisisitiza Mgonya.

 

Akizungumzia wajibu na jukumu la  Ofisi ya Msajili wa Hazina katika mradi huo, Mgonya alisema pamoja na majukumu mengine kama yalivyoanishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370, Ofisi ina jukumu la kuishauri Serikali na kusimamia uwekezaji wake katika Taasisi, Mashirika na Wakala za Serikali.

 

Na kwamba, katika mradi wa shamba la Mngeta,  Ofisi yake inatekeleza moja ya matakwa ya Sheria, akisema walianza kwa kuishauri Serikali kulinunua shamba hilo na kupendekeza Shirika la SUMA JKT ambalo pia linasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina liwe mwendelezaji wa shamba la Kilombero.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Absolomon Shausi ameishukuru Serikali kwa hatua ya kulinunua na kuwakabidhi shamba hilo lenye manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo linalozunguka na Taifa kwa ujumla.  Aidha, Brigedia Jenerali Shausi ameahidi kulisimamia na kuliendeleza shamba hilo ili kufikia malengo ya uwekezaji wa Serikali.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, aliyekuwa Mfilisi wa Shamba hilo, Mlola ameishukuru Serikali kwa ushirikiano na kukamilisha kwa wakati makubaliano yote yaliyofikiwa katika zabuni husika mpaka kufikia hatua ya mwisho ya makabidhiano na hivyo kuahidi kutoa ushirikiano wakati wote.

 

Ends