SERIKALI kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Shirika la Posta nchini lengo ikiwa ni  kuongeza uzalishaji na kutekeleza majukumu yake liweze kuendana na lengo la uanzishwaji wake kwa mujibu wa Sheria iliyounda Shirika hilo.

Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa na Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto wakati akifunga mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center, jijini Dodoma.

Msajili huyo wa Hazina  amesema Serikali inatambua mchango wa Shirika la Posta katika kuwahudumia wananchi hasa katika sekta ya Mawasiliano, ndiyo maana inaendelea kuliongezea nguvu Shirika ili liendelee kutoa huduma stahiki na zinazoendana na mahitaji ya wakati ya wananchi.

Itakumbukwa kuwa mwaka jana, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliamua kulipunguzia mzigo Shirika wa kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki baada ya Serikali kuchukua jukumu hilo na pia Serikali ililirejeshea Shirika kiasi cha Bilioni 7.9 ikiwa ni fedha lilizotumia kuwalipa wastaafu hao kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1994 2006 na 2015-2020 lengo likiwa ni kuliongezea ufanisi Shirika hilo.

“Serikali iliamua kurejesha Shilingi bilioni 7.9  ikiwa ni fedha walizolipwa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki ili kuweka mazingira wezeshi kwa Shirika kuongeza uzalishaji na kutekeleza majukumu yake”. Amesema Mgonya.

Aidha, Msajili wa Hazina amelitaka Shirika la Posta kuzitumia fedha hizo kwa kuzingatia maelekezo na malengo ya fedha hizo katika kuboresha vitendea kazi vya Shirika, pia amewataka watendaji wa Shirika hilo kuongeza ubunifu ili kuleta tija katika kuongeza pato la Taifa na hatimaye kuweza kutoa gawio kwa Serikali.

Sambamba na hilo, ameahidi Ofisi yake itaendelea kushirikiana na Shirika la Posta katika utatuzi wa changamoto za kiuendeshaji na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kushirikiana na Serikali ikiwemo suala la Mtaji kwa Shirika na malimbikizo ya madeni ya kodi ya muda mrefu (ya shilingi  Bilioni 26 yanayotakiwa kuchukuliwa na Serikali).

Akizungumza wakati akimkaribisha Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Msaidizi Ufuatiliaji na Tathmini  wa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Elisa Mbise kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema kuwa, Serikali iko tayari kuliboresha Shirika la Posta ili liongeze tija kwa Taifa na kuwataka watendaji wa Shirika kuonesha uwezo wa kutumia rasilimali walizonazo ili Serikali iendelee kuona umuhimu wa kuliimarisha  Shirika hilo kiutendaji.

“Onesheni uwezo wa kutumia rasilimali mlizonazo ili Serikali ione umuhimu wa kuendelea kuwaongezea  mtaji muweze kuboresha utendaji wenu ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za Posta”. Alisema Mbise.

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa TPC,  Macrice Mbodo amesema katika mkutano huo, wajumbe wamepatiwa mafunzo ya huduma kwa mteja; wamepitia Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (2022/33 – 2025/26) unaojikita kuifanya “Posta ya Kidijitali kwa maendeleo endelevu” pamoja  na kupitia Mapendekezo ya Mpango Mkakati mpya wa nane wa kibiashara wa miaka mitano (2022/23 – 2026/27).

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Baraza Afisa Masoko Mwandamizi kutoka Zanzibar, Bi Halima Abdulla Hamad amemshukuru Msajili wa Hazina kwa kutenga muda wake kufunga Baraza hilo, na kuahidi kutekeleza yote waliyoyajadili katika kikao hicho ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Shirika

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mbunge wa Viti Maalum (Wafanyakazi), Mhe. Dkt. Alice Karungi Kaijage, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kitaifa wa Bara na Zanzibar pamoja na Viongozi wa Shirika la Posta kwa ngazi ya Makao Makuu na Mikoa.