Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA MSAJILI WA HAZINA

Mkurugenzi Utawala, Ofisi ya Msajili wa Hazina afariki
23 Dec, 2024
Mkurugenzi Utawala, Ofisi ya Msajili wa Hazina afariki

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw. Amos Nnko amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro.

 

Ajali hiyo iliyotokea siku ya Jumapili, Desemba 22, 2024 majira ya mchana, pia ilipelekea kifo cha binti yake wa kwanza, Maureen Nnko.

 

Pia katika ajali hiyo, mke wa marehemu Bi. Agnes Nnko na watoto Marilyn, Melvin na mwanafamilia mwingine, Sylvana, walijeruhiwa.

 

Majeruhi wanaendelea kupata matibabu katika hospitali ya KCMC na Mawenzi.

 

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu Jumatatu, Desemba 23, alisema kifo cha Bw. Nnko ni pigo kubwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taifa kwa ujumla.

 

Bw. Mchechu alimuelezea marehemu Nnko kama mchapakazi, muadilifu na mtu wa watu.

 

“Tumepokea taarifa za kifo cha Nnko kwa masikitiko makubwa sana. Tumepoteza nguzo muhimu,” alisema Bw. Mchechu.

 

Sanjari na hilo, alitoa pole kwa familia ya marehemu huku akiwaombea majeruhi wa ajali hiyo uponyaji wa haraka.

 

Bw Mchechu alisema taratibu za mazishi zinaendelea kuratibiwa huko Tengeru, Arusha kwa ushirikiano wa familia ya marehemu na  Ofisi ya Msajili wa Hazina.