Na Mwandishi Maalumu, Dodoma

UONGOZI wa Shirika la Posta Tanzania umetakiwa kutilia mkazo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili liweze kuendana na matakwa ya dunia ya sasa, hasa katika utoaji wa huduma.

Aidha, shirika limetakiwa kuchangamkia fursa za utandawazi kwa kutanua wigo wa biashara hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika la Posta linapambana kujiimarisha kiuchumi, lakini pia liangalie namna ya kupunguza gharama za uendeshaji ili matunda yake yaweze kuonekana.

Mwito huo ulitolewa hivi karibuni jijini Dodoma na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alipokuwa anafunga mafunzo ya siku tano ya uongozi na utendaji kazi wa viongozi wa Shirika la Posta Tanzania.

Alisema mafunzo waliyoyapata yakitumika vyema yatakuwa na tija na kuongeza faida kwa shirika, huku akiwataka wanufaika wa mafunzo kushusha elimu waliyoipata kwa wafanyakazi hadi wa ngazi ya chini ili kujenga mtazamo wa pamoja katika kulitumikia shirika.

“Niwapongeze kwa kuandaa utaratibu wa kuwa na mafunzo haya ndani ya Shirika. Mafunzo ni uhai wa Shirika, hivyo niwaase msiache kuendelea kupeana mafunzo kila mara inapohitajika kuanzia viongozi wa juu wa Shirika hadi mhudumu ili muweze kwenda pamoja kutekeleza yale mliyokubaliana,” alisema.

Akizungumzia umuhimu wa teknolojia, alisema dunia kwa sasa imeelekea zaidi kwenye matumizi ya Tehama kwa ujumla, hivyo anaamini kupitia mafunzo hayo Shirika litatilia mkazo zaidi katika eneo la teknolojia ili liendane na matakwa ya dunia ya sasa hasa eneo la kutoa huduma.

“Naamini mmeweza kuongeza weledi katika kulihudumia soko kwenye mabadiliko ya kiteknolojia yanayokwenda kwa kasi, hivyo nanyi hamna budi kuwa na kasi katika yale tunayolenga kuyafanya huku tukizingatia ubunifu na unyumbulifu,” alisema.

 

Alisema pamoja na mikakati mizuri ya kulinyanyua shirika, uongozi unapaswa pia kuangalia jinsi ya kupunguza gharama za uendeshaji sambamba na kuongeza mapato ili liweze kutoa gawio na michango mingine kwa Serikali kila mwaka, akisisitiza kuwa, dhamira ya uwekezaji wa Serikali katika Taasisi, Mashirika na makampuni ambako imeweka hisa zake ni kupata faida ambayo itarejea serikalini ili nayo iweze kutoa huduma mbalimbali kwa jamii.

 

Aligusia pia jinsi shirika linavyoaminiwa, akitolea mfano mkataba wa biashara ya usafirishaji wa sampuli za damu ulioingiwa baina ya Posta na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwamba kazi waliyopewa ni nyeti na kuwataka kuwa makini wakati wa utelekezaji wake ili kuhakikisha sampuli hizo zinafika kwa wakati na usalama.

 

“Katika hili la usafirishaji wa damu, uaminifu na uchapakazi wa pamoja utaimarisha huduma hii na huduma zingine za Posta hivyo kuleta mabadiliko chanya na maendeleo ya shirika kwa ujumla,” alisema Mbuttuka.

Pamoja na mambo mbalimbali yaliyofundishwa, viongozi hao walijifunza pia juu ya uboreshwaji wa mifumo ya Shirika la Posta, ufungaji wa mahesabu, njia za uendeshaji biashara na huduma za Posta, jinsi ya kukuza biashara, na kujijengea ubunifu na fikra za kibiashara kwa viongozi.

Mafunzo yamegusia pia mfumo wa Rasilimali watu ndani ya shirika, mikataba ya kiutumishi na watumishi ndani ya shirika, na jinsi ya kushughulikia kesi na migogoro ya wafanyakazi.

Mbuttuka alisema hayo yote yakifanyiwa kazi, yatasababisha Shirika la Posta kuongeza kasi ya uzalishaji na mapato ya shirika na hivyo kulifanya kuendana na mageuzi ya kiuchumi yaliyo sasa, ya uchumi wa kati.

 

TAMATI